Habari Mseto

Wananchi wakamata na kutandika polisi walevi kisiwani

December 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

KALUME KAZUNGU na JOSEPH NDUNDA

POLISI kisiwani Lamu walilazimika kutimua umati uliokuwa ukiwatandika wenzao wawili waliokamatwa na kufungwa kwa kamba na raia kwa madai ya kuhangaisha watu wakiwa walevi.

Maafisa hao yadaiwa walikuwa wamekunywa pombe ya mnazi katika kijiji cha Mararani kinachotambulika kwa biashara ya vileo vya kienyeji.

Yadaiwa wakiwa wanapepesuka, polisi hao waliovaa kiraia walianza kuhangaisha wakazi kwa kuwalazimisha kujitambulisha kwa kuonyesha vitambulisho vyao vya kitaifa.

Waliokaidi amri ya maafisa hao walitandikwa, jambo lililowakasirisha wakazi ambao walikusanyika na kuwapiga maafisa hao. Baadaye waliwafunga kamba mikononi na kuwaitia polisi wenzao kuwachukua.

Kiongozi wa Nyumba Kumi kijijini humo, Bw William Diwa, alisema kundi la polisi waliobeba bunduki na marungu liliwasili na kuanza kuwapiga wanakijiji kabla ya kuwakamata zaidi ya 10 na kuwapeleka kituo cha polisi cha kisiwa cha Lamu.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alithibitisha tukio la kupigwa kwa maafisa wa polisi eneo la Mararani na akasema tayari uchunguzi kuhusiana na tukio hilo umeanzishwa.

“Mmoja wa polisi anadai kuibiwa Sh7,000 wakati wa tukio hilo ilhali kijana mmoja akidai kupokonywa simu yake ya mkononi na maafisa hao. Wote wamekamatwa na kufikishwa kituoni kuandikisha taarifa huku uchunguzi ukiendelea,” akasema Bw Macharia.

POLISI WATEKAJI

Jijini Nairobi, Idara ya DCI jana ilipata agizo la mahakama la kuwazuilia maafisa wawili wa polisi waliokamatwa katika mtaa wa Eastleigh mnamo Jumamosi kwa jaribio la kumteka nyara polisi mwenzao.

Hakimu Mwandamizi wa Makadara, Stephen Jalang’o aliruhuru polisi kuwazuilia Abdikadir Daiche na Ali Shukri Galgalo katika kituo cha polisi cha Pangani kwa siku saba ili wakamilishe uchunguzi.

Daiche ni afisa anayefanya kazi katika kituo cha polisi cha Muthaiga huku Galgalo akihudumu katika kituo kidogo cha polisi cha Quarry eneo la Embakasi.

Wawili hao walikamatwa gari wanalodaiwa kuteka nyara lilipokwama mwendo was saa saba za usiku.

Wanadaiwa walikuwa wameteka gari la dereva wa Uber ambaye ni afisa mwenzao wa wa polisi mara baada ya kushukisha abiria kwenye barabara ya Juja, eneo la Pangani.

Idadi ya maafisa wa usalama wanaokamatwa kwa kuhusika katika visa vya uhalifu imekuwa ikiongezeka katika maeneo mbalimbali ya nchi.