Barcelona kileleni La Liga baada ya kuipiga Atletico
Na MASHIRIKA
MADRID, UHISPANIA
LIONEL Messi alifunga bao la dakika za mwisho na kuwasaidia Barcelona kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Atletico Madrid uwanjani Wanda Metropolitano mnamo Jumapili.
Ni matokeo ambayo yaliwarejesha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kileleni mwa jedwali kwa alama 31 sawa na watani wao wa tangu jadi, Real Madrid.
Messi alimzidi maarifa kipa Jan Oblak wa Atletico kunako dakika ya 86 na kupachika wavuni bao lake la 11 kutokana na mechi 10 hadi kufikia sasa katika kivumbi cha La Liga.
Awali, Barca ndio walioonekana kuzidiwa ujanja katika takriban kila idara huku kipa Marc-Andre ter Stegen akijipata katika ulazima wa kujituma vilivyo kupangua makombora ya Mario Hermoso na Alvaro Morata.
Real chini ya kocha Zinedine Zidane, waliwapokeza Alaves kichapo cha 2-1 mnamo Jumamosi na kuchupa hadi kileleni mwa jedwali huku ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Sevilla dhidi ya Leganes ukiwadumisha katika nafasi ya tatu kwa alama 30.
Real Sociedad wanafunga orodha ya nne-bora kwenye msimamo wa jedwali la La Liga kwa alama 26 sawa na Athletic Bilbao.
Mashambulizi ya Hermoso na Morata yaliwazindua Barcelona ambao walirejea katika kipindi cha pili kwa matao ya juu.
Ushirikiano mkubwa kati ya Messi na Ivan Rakitic ulizalisha fursa ilimsaza Gerard Pique akiwa peke yake na Oblak, ila mpira aliouelekeza langoni ukabusu mlingoti wa goli.
Mabadiliko muhimu yaliyofanywa na kocha Diego Simeone katika kipindi cha pili yalibadilisha kasi ya mchezo kwa upande wa Atletico ambao walipoteza nafasi nyingi za wazi kabla ya chombo chao kuzamishwa na Messi ambaye Jumatatu alitoana jasho na Cristiano Ronaldo na Virgil van Dijk kwenye hafla ya kutawazwa kwa Mwanasoka Bora wa Mwaka jijini Paris, Ufaransa.
Ufanisi huo wa Barcelona unamaanisha kwamba Atletico kwa sasa wameshindwa kusajili ushindi katika jumla ya michuano 19 iliyopita dhidi ya Barcelona.
Hii ni rekodi ambayo vijana wa kocha Simeone wameshindwa kuivunja tangu Februari 2010.
Kufikia sasa, ni pengo la alama sita ndilo linalotamalaki kati ya Barcelona na Atletico waliotawazwa wafalme wa La Liga kwa mara ya mwisho mnamo 2013-14.
Katika matokeo mengine Athletic Bilbao waliwapepeta Granada 2-0, Espanyol wakacharazwa 4-2 na Osasuna nao Getafe wakawaponda Levante 4-0.