Waliokwama mtoni siku tatu wasimulia masaibu
Na PIUS MAUNDU
WANAUME watatu waliokuwa wamekwama katika kisiwa kilichoko katikati mwa Mto Athi unaopitia kijijini Yikivuthi, Kaunti ya Makueni tangu Jumamosi, wameelezea masaibu yao baada ya kuokolewa Jumatatu.
Mutuku Tila, 38, Muteti Kiambi, 35, na Muinde Kasuu, 37, walienda kisiwani hapo kuangalia mizinga yao ya nyuki kabla ya maji kuongezeka ghafla.
Watatu hao ambao hujikimu kwa kuchoma makaa na kurina asali waliripotiwa na familia zao kutoweka Jumamosi. Siku moja baadaye walionekana wakiwa wamesimama juu ya mwamba kisiwani hapo.
Wakazi waliripoti kwa polisi ambao waliwasili jana kwa helikopta na kuwaokoa.
“Tulienda kisiwani hapo kuangalia mizinga yetu kabla ya maji kuongezeka. Tulikuwa tukila asali kwa siku tatu,” akasema Bw Kiambi baada ya kushuka kutoka kwenye helikopta.
Walisema walikuwa wakilala juu ya mwamba na kuwa uwepo wa jamaa zao na wakazi kando ya kingo za mto huo uliwatia nguvu za kuendelea kungojea msaada.
“Jumapili, tulikuwa tumeamua kuogelea lakini chifu akatwambia tusijaribu kufanya hivyo kutokana na hofu kwamba tungesombwa na mafuriko,” akasema Bw Kasuu.
Kulingana na Kamishna wa Makueni, Mohammed Maalim, jumla ya watu 10 wamefariki katika kaunti hiyo kutokana na mafuriko hivi karibuni.
Wengi walifariki wakijaribu kuvuka mito iliyokuwa imejaa maji.
Miongoni mwao, watatu waliaga dunia katika eneo la Kilungu wikendi iliyopita.
Wakati huo huo, mwanamume mwingine aliyekuwa amekwama katika maporomoko ya 14 Falls ya mto huo wa Athi River katika eneo la Thika, Kaunti ya Kiambu aliokolewa Jumapili jioni kwa helikopta ya polisi.
Vincent Musila, ambaye ni mvuvi, alikuwa ameenda eneo hilo kwa shughuli zake za kila siku maji yalipoongezeka na akashindwa kurudi kingoni. Alikwama kwa siku tatu.