• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
Mafuriko yazidi kusomba nyumba za wakazi

Mafuriko yazidi kusomba nyumba za wakazi

Na WAANDISHI WETU

WATU saba walifariki katika visa vitatu tofauti kutokana na mvua inayoendelea.

Wawili walipatikana wamefariki ndani ya mto Ngong, jijini Nairobi, wawili katika kaunti ya Taita Taveta na watatu katika kaunti ya Makueni.

Mwili wa mwanamume uligunduliwa na vijana waliokuwa wakiondoa taka zilizoziba daraja la Kaiyaba/ Hazina mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba, eneo bunge la Starehe.

Katika kisa cha pili, mwili wa mwanamke ulipatikana ndani ya mto huo katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kwa Reuben eneo la Embakasi Kusini.

Kwingineko, mamia ya watu walilazimika kulala kwa marafiki na majirani baada ya nyumba zao kusombwa na maji baada ya mto Ngong kuvunja kingo zake.

Mitaa ya mabanda iliyoathirika zaidi ni pamoja na Mukuru-Kaberira, Mukuru-Commercial, Mukuru-Fuata Nyayo, Mukuru-Kenya Wine, Mukuru-Mariguni, Mukuru-Kaiyaba na Maasai Village.

Katika kaunti ya Taita Taveta, wakazi wa kijiji cha Ghazi jana walikuwa wakiendelea kusaka mwili wa mtu mmoja kati ya wawili waliouawa na mafuriko.

Mmoja wa wakazi hao, Bi Sylvia Mwakuja, alisema kuwa mwanamume huyo alibebwa na maji baada ya mto wa Mwakajo kufurika.

“Walikuwa wakielekea nyumbani usiku akiwa na wenzake wawili wakati kisa hicho kilipotokea,” akasema.

Wawili hao waliponea mauti baada ya kunusurika kutoka kwa mto huo.

Katika eneo la Wundanyi, zaidi ya familia 41 zimesalia bila makao baada ya nyumba zao kuharibiwa na maporomoko ya udongo katika vijiji vitatu vya eneo hilo.

Katika kaunti ya Makueni, Kamishna Bw Mohammed Maalim alisema wanaume watatu walifariki wikendi, na kufikisha idadi ya waliouawa tangu mvua ianze kuwa kumi.

“Wengi wa waliozama maji walikuwa wakijaribu kuvuka mito iliyofurika. Watatu, akiwemo mtoto wa kike wa miaka sita, walikufa katika eneo la Kilungu,” akasema.

Wanaume wengine watatu walizungukwa na maji kutoka Mto Athi, unaopitia kijiji cha Yikivuthi kwa siku ya tatu jana huku wakiwa hawajaokolewa.

Watatu hao, Mutuku Tila, Mutei Kiambi na Muinde Kasuu walizungukwa na maji Jumamosi, mto Athi ulipofurika ghafla.

Ripoti za SAMMY KIMATU, LUCY MKANYIKA na PIUS MAUNDU

You can share this post!

Serikali kudukua simu za wanahabari wanaoikosoa

Dereva wa teksi ashtakiwa kumbaka mteja na kuiba mali yake

adminleo