• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
IEBC mbioni kuhakikisha demokrasia na mada kuhusu uchaguzi zinapewa zingatio shule za msingi

IEBC mbioni kuhakikisha demokrasia na mada kuhusu uchaguzi zinapewa zingatio shule za msingi

Na MISHI GONGO

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeanzisha mikakati ya kutaka kuingizwa kwa somo la demokrasia na uchaguzi katika shule za msingi ili kuzima ukabila na machafuko yanayoweza kusababishwa na michakato ya uchaguzi siku zijazo.

Akizungumza Jumanne katika chuo cha serikali cha mafunzo ya ushuru kwenye kongamano la walimu wakuu mjini Mombasa, Mkurugenzi wa IEBC anayehusika na Elimu kuhusu Uchaguzi, Ushirikiano na Mawasiliano Bi Immaculate Kassait amesema somo hilo litawapa wanafunzi mwanga kuhusu uongozi bora.

“Tumekuwa tukishuhudia machafuko wakati wa uchaguzi katika nchi yetu. Somo hili litawaelimisha watoto kuhusu umuhimu wa demokrasia na uongozi bora katika taifa,” ameeleza Bi Kassait.

Amesema kuwa somo hilo litawafunza wanafunzi wa shule za msingi kuhusu hatua muhimu na namna ya kupiga kura, umuhimu wa kupiga kura na umuhimu wa kuchagua kiongozi kutokana na ubora wake na si kwa misingi ya kikabila.

“Tunataka kukuza jamii ambayo itakuwa inafikiria katika misingi ya ubora wa kitaifa na sio tu jamii yao au eneobunge wanalotoka,” amesema mkurugenzi huyo.

Mwenzake wa kutoka tume hiyo Bw Lawrence Baraza amesema bado wanajadiliana na Wizara ya Elimu kuhusu vipi somo hilo litaingizwa katika mfumo mpya unaojikita katika uamilifu.

“Tutajadiliana kujua iwapo litakuwa ni somo au mada katika mojawapo ya masomo wanayofunzwa,” ameeleza Bw Baraza.

Ameeleza kuwa somo hilo litafunza sehemu ya demokrasia na elimu kuhusu uchaguzi na kupiga kura.

Kwa sasa tume hiyo inasimamia uchanguzi unaoendeshwa katika baadhi ya shule za msingi kuchagua viongozi.

“Tunatembelea shule za msingi kuona jinsi wanavyoshawishi wenzao kuwachangua na tunawaongoza namna wanavyopaswa kutekeleza uchaguzi huo,” ameeleza Bw Baraza.

Walichagua shule za msingi kuhamasisha wanafunzi kwa sababu wao ndio viongozi wa kesho.

Mradi huo unadhaminiwa na serikali ya Canada (Kanada), Wizara ya Elimu na Taasisi ya Kukuza Mitaala Nchini (KICD).

You can share this post!

BBI: Jiandae kwa kivumbi, Kamket amwambia Ruto

Korea Kaskazini yaahidi Trump ‘zawadi ya Krismasi’

adminleo