Korea Kaskazini yaahidi Trump ‘zawadi ya Krismasi’
Na AFP
KOREA Kaskazini imeadhimisha mwanzo wa msimu wa sherehe za Krismasi kwa kuiahidi Amerika “zawadi ya Krismasi’” iwapo haitapiga hatua yoyote katika kufufua majadiliano kuhusu nuklia mnamo Disemba.
Mnamo Aprili, Kim Jong-un, kiongozi wa Korea Kaskazini aliweka makataa ya mwisho wa mwaka kwa Washington kuonyesha uwezo wake wa kuruhusu mabadiliko katika nafasi yake, lakini maafisa wa Amerika wamefafanua makataa hayo kama yasiyo halisi, wakionekana kupuuzilia mbali umuhimu wake.
Katika taarifa mpya kutoka Pyongyang, mojawapo wa maonyo kadha yaliyotolewa kupitia vyombo vya habari, Ri Thae Song, naibu waziri wa masuala ya kigeni anayesimamia mahusiano ya Amerika, aliishutumu Amerika kwa kujaribu kuchelewesha mazungumzo ya kukomesha silaha za nuklia kabla ya uchaguzi wa urais Amerika mwaka ujao.
“Majadiliano yanayopigiwa debe na Amerika kwa hakika si chochote ila hila za kipumbavu za kuiweka DPRK ikiwa imefungika katika majadiliano na kuitumia kufaidi hali ya kisiasa na uchaguzi Amerika,” alisema akirejelea jina rasmi linalotumiwa kwa Korea kaskazini.
Miezi michache iliyopita imegubikwa na misururu ya majaribio ya silaha kutoka Korea Kaskazini.