Habari Mseto

Walimu wahimizwa kuunga mkono mfumo wa CBC

December 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

WALIMU wamehimizwa kuunga mkono mfumo wa elimu wa uamilifu (CBC) kwani mfumo huo ulianzishwa kwa wakati unaofaa na utaboresha elimu.

Akiwahutubia zaidi ya walimu 7,000 wa shule za msingi mjini Mombasa, mwenyekiti wa kitaifa wa Muungano wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (Kepsha) Bw Nicholas Gathemia amesema kuwa mfumo huo utawafanya wanafunzi kuwa wenye makini zaidi na wataweza kukifanya kile walichokisoma.

“Mfumo wa CBC una manufaa sana kwa watoto wetu; tukiuunga mkono tutawawezesha kupata ujuzi wa kujitegemea maishani,” amesema Gathemia.

Mkutano huo wa walimu wa msingi umekamilika leo Alhamisi.

Zaidi ya walimu 7,500 wakuu wanahudhuria mkutano huo wa siku nne ambao nia yake ni kuzungumzia usimamizi wa shule ambao unafanywa na walimu wakuu.

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kukuza Mitaala Nchini (KICD) Dkt Julius Jwan amewatahadharisha wazazi pamoja na walimu dhidi ya kuvitumia vitabu ambavyo havijaidhinishwa na KICD.

“Tungewataka wazazi kuvinunua vitabu ambavyo vimeorodheshwa katika Orange Book,” amesema Dkt Jwan.

Vitabu hivyo vimekaguliwa na wataalamu ambao ni pamoja na walimu mbalimbali.