• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Jukwaa jipya kusaidia wanahabari kuanika maovu katika jamii

Jukwaa jipya kusaidia wanahabari kuanika maovu katika jamii

NA FAUSTINE NGILA

MRADI mpya umezinduliwa jijini Nairobi kukuza vipawa vya wanahabari, wasanii na wanaharakati kwa lengo la kuinua viwango vya kuikosoa jamii na kubuni mbinu mpya kwa vyombo vya habari kujisitiri kifedha wakati huu wa mageuzi ya kiteknolojia.

Jukwaa hilo kwa jina Baraza Media Lab lenye ofisi zake katika jumba la Keystone Park, Riverside, Nairobi pia litawashirikisha wanafilamu, wanablogu, waigizaji, waandishi na wanafunzi wa uanahabari kuvumisha ubunifu katika kazi za uanahabari.

Juhudi hizo zimefadhiliwa na shirika la Luminate linalopiga jeki jitihada za kuleta mageuzi duniani kuifaa jamii. Kenya ni taifa la kwanza duniani kufaidika na mradi kama huu, kati ya mataifa 18 yaliyo chini ya mwavuli wa Luminate.

“Tunajizatiti kuimarisha tasnia ya uanahabari nchini kwa kuwahusisha watu wote kupambana na sera mbovu za kisiasa, kiuchumi na kijamii na kuleta uaminifu katika habari zinazoenezwa na wanahabari wa Kenya,” akasema Christine Mungai, msimamizi wa mradi huo.

Bi Ory Okolloh, meneja mkurugenzi wa Luminate barani Afrika alipoonya kuhusu misemo ya kuigawanya jamii. Picha/ Faustine Ngila

Baraza Media Lab itashirikiana na kampuni ya kuwaleta pamoja wataalamu wa sekta mbalimbali, Metta kuendesha ajenda ya kuchapisha na kupeperusha habari na Makala yanayoihusu jamii.

“Tumeshuhudia uanahabari nchini Kenya ukisombwa na mawimbi ya dijitali, siasa zikigawanya jamii, ufisadi ukipenyeza mizizi hadi mashinani na visa vya mauaji, wizi na ubakaji vikiongezeka. Mradi huu unalenga kuanika maovu haya,” akaongeza.

Meneja mkuu wa Metta Bw Maurice Otieno alisema hii ni fursa kwa wanahabari wa Kenya kunoa makali yake kwa kushirikiana na wanaharakati, wanafilamu tajika na wasomi.

“Kushirikiana kutaiunganisha jamii zaidi na kuisaidia kuikuza tunapoangazia hali za watu za kimaisha, na jinsi sera za serikali zinawaathiri,” akasema.

Iliibuka kuwa misemo ya kisiasa kama ‘mtajua hamjui’ na ‘mambo kwa ground ni different’ imechangia pakubwa kuigawanya jamii, huku mirengo ya kisiasa ikieneza chuki na uhasama.

“Ni wakati wa kukemea misemo hii kwa kuwa inaeneza jumbe hatari kwa uwiano wa jamii. Ni shinikizo za kisiasa na kibiashara ambazo zisipozimwa zitaua ndoto za vijana wengi,” akasema Bi Ory Okolloh, meneja mkurugenzi wa Luminate barani Afrika.

Sekta ya uanahabari duniani inakumbwa na misukosuko, huku baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara kama Donald Trump na Elon Musk wa Amerika wakiwa na usemi mkubwa kuliko baadhi ya mataifa na vyombo vya habari.

Mwanahabari mwenye tajriba kubwa ya kuripoti habari za kimataifa Bi Uduak Amimo alisema jukwaa hilo pia litasaidia wahariri wa magazeti, redio na runinga kufikiria upya kuhusu maovu yanayofanyika ndani ya afisi za uanahabari.

Bi Uduak Amimo alipohutubu katika uzinduzi wa Baraza Media Lab mtaani Riverside Desemba 5, 2019. Picha/ Faustine Ngila

“Iweje utaanika habari za dhuluma za kimapenzi na malipo duni wakati zimekithiri ndani ya idara yako unayosimamia? Ni wakati wa kubadilisha dhana hizi, na Baraza Media Lab ni jukwaa mwafaka,” akasema.

Pia, iliibuka kuwa baadhi ya wanahabari huegemea kwa mirengo ya kisiasa kutokana na makabila ya na hivyo kukosa kukosoa wanasiasa kutoka mirengo hiyo, hali inayoumiza lengo kuu la uanahabari.

Mradi huo utaanza na hafla ya kutambua habari zilizotesa anga katika mwaka huu wa 2019 itakayoandaliwa katika ofisi zake hapo Desemba 17.

You can share this post!

Kenya yapoteza tena Dubai Sevens

Maprofesa wenye tajiriba pevu wanahitajika vyuoni –...

adminleo