• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Inatukera sana kuona hela zetu zikitafunwa na mafisadi – Walemavu

Inatukera sana kuona hela zetu zikitafunwa na mafisadi – Walemavu

Na SAMMY KIMATU

MAKUMI ya walemavu walikongamana katika ukumbi wa kanisa la Katoliki la Soweto kwenye mtaa wa Kayole ulio katika Kaunti ndogo ya Embakasi Mashariki, Kaunti ya Nairobi.

Aidha, walikuwa wakisherehekea Siku ya Kimataifa ya Watu Walemavu (International Day of Persons Living with Disabilities 2019).

Mada ya mwaka huu ilikuwa ni, “The Future is Accessible.”

Msafara wa walemavu siku ya kuadhimisha Siku ya Walemavu Duniani katika hafla iiyofanyika katika Kanisa Katoliki la Soweto mtaani Kayole, kwenye Kaunti ya Nairobi. Picha/SAMMY KIMATU

Walioshiriki walikuwa ni pamoja na walemavu wa akili, miguu, vipofu, viziwi na bubu miongoni mwa wengine.

Kulikuwamo watoto wachanga waliobebwa na wazazi wao huku wengine wakisukumwa wakiwa kwenye viti vyenye magurudumu.

Palikuwamo pia vijana, kina mama kwa wazee.

Kabla ya kuingia ukumbini, washiriki walikuwa na gwaride uwanjani wa kanisa hili huku wakiandamana na bango lenye maandishi (IDDD 2019).

Wanasarakasi na mbwembwe zao wakitumbuiza washiriki Siku ya Walemavu Duniani katika hafla iiyofanyika katika Kanisa Katoliki la Soweto mtaani Kayole, kwenye Kaunti ya Nairobi. Picha/SAMMY KIMATU

Baada ya kuingia ukumbini, walifungua mkutano wao kwa maombi kabla kipindi cha kutumbuiza kuanza.

Walemavu wawil wakike waliwaacha wengi vinywa wazi walipotumbuiza kwa wimbo wakitumia ishara na lo! Nusura watu wavunjike mabavu kuwaona akina dada hao walivyonengua viuno vyao.

Baada ya mabinti hao kutoka jukwaani, kulijimwaya kundi la vijana waliobebea katika sanaa ya sarakasi.

Katika wakati wa kutoa kauli zao afisa wa programu katika Chesire Disability Services Kenya (CDSK) ambao ndio walikuwa wenyeji, Bw George Shimanyula, alisema walemavu wanahitaji nafasi yao katika jamii.

Wanasarakasi na mbwembwe zao wakitumbuiza washiriki Siku ya Walemavu Duniani katika hafla iiyofanyika katika Kanisa Katoliki la Soweto mtaani Kayole, kwenye Kaunti ya Nairobi. Picha/SAMMY KIMATU

“Tumepiga hatua mbele zaidi ambapo walemavu wanapata sauti ukilinganisha na miaka ya hapo awali kufuatia ushirikiano na mashirika kama vile Light for the World na Liliane Fodes kutoka Uholanzi miongoni mwa wengine,” Bw Shimanyula akasema.

Aliongeza kwamba walemavu wakati mwingine huonekana kama hawajiwezi na kudaiwa ni wanyonge lakini wahitaji kupewa haki zao za kimsingi kama watu wale wengine, Bw Shimanyula akasisitiza.

Kwa niaba ya walemavu wenzake, Bw Benard Opiyo kutoka mradi wa Able Entreprise alisema wanachama wao hupata mapato baada ya kuinuliwa na wafadhili kama vile CDSR.

WALEMAVU wakiadhimisha Siku ya Walemavu Duniani katika hafla iiyofanyika katika Kanisa Katoliki la Soweto mtaani Kayole, kwenye Kaunti ya Nairobi. Picha/SAMMY KIMATU

“Ufisadi unatukera na kutufinya wakati pesa zinaingia kwa mifuko ya watu binafsi huku tukibakia maskini hoe hae na walala hoi,” Bw Opiyo akasema.

Aliomba wafisadi wachukuliwe hatua kali kisheria ili wengine walio na kiu cha kupora mali ya umma wawe na funzo na wakome.

Kuhusu BBI, walemavu wanaomba ile asilimia tano ya nafasi za kazi wapewe kama ilivyo katika katiba.

“Kuna umuhimu wa walemavu kuwasomesha wenye viwanda ili wapate kuyaelewa na kuyatilia maanani matakwa yao,” Bw Opiyo akasema.

You can share this post!

Uokoaji waendelea kunusuru waliokwama jengoni Tassia

Waathiriwa wa mafuriko kupewa makao mapya

adminleo