Waathiriwa wa mafuriko kupewa makao mapya
Na WAANDISHI WETU
SERIKALI kuu na za kaunti ziko mbioni kuwapa makao mapya waathiriwa wa mafuriko katika maeneo yaliyoathirika zaidi na mvua kubwa inayotabiriwa itaendelea kunyesha mwezi huu, kabla shule zifunguliwe mwezi ujao.
Waziri wa ugatuzi, Bw Eugene Wamalawa alisema kufikia wikendi, kaunti ya Pokot Magharibi ndio iliathirika zaidi.
Akiongea mjini Makutano ambapo alisambaza chakula na vifaa kwa waathiriwa, alisema miongoni mwa msaada utakaotolewa ni vifaa vya kujenga nyumba kwa wale ambao nyumba zao zilibomolewa wakati wa mafuriko.
“Maeneo mengi nchini yameshuhudia mafuriko na tumepoteza watu watu wengi. Katika Kaunti ya Pokot Magharibi tumepoteza zaidi ya watu 50. Nyumba ziliharibiwa na wanyama kusombwa na mafuriko. Katika Kaunti ya Makueni tulipoteza maisha 13. Tunataka kuhakikisha kuwa wale wote walipoteza wapendwa wao wanapata msaada,” alisema.
Waziri aliongeza kuwa, serkali itaanza ujenzi wa nyumba za waathiriwa haraka iwezekanavyo ili watulie makwao kabla ya shule kufunguliwa kwani wengi waliokosa makao wamekita kambi shule tofauti.
“Shule tatu zimegeuzwa kuwa kambi katika eneo hili na tunataka wakati shule zinafunguliwa, waathiriwa wawe makwao,” alisema.
Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta nayo ilisema itajenga nyumba mpya kwa waliopoteza makao yao wakati wa mafuriko hayo.
Kuna familia zaidi ya 300 ambazo bado zimekita kambi katika Shule ya Msingi ya Voi baada ya nyumba zao kuharibiwa na mvua.
Katika Kaunti ya Kiambu, kijiji cha Giciiki, Gatuanyaga, Thika Mashariki, imegeuka mahame baada ya wakazi wa eneo hilo kuhama na mali zao kufuatia mafuriko.
Walidai kuwa kwa muda wa wiki moja sasa mvua kubwa imewakosesha amani katika makazi yao huku wakilazimika kutafuta maeneo salama ili kujikinga na mvua hiyo.
Walizidi kueleza kuwa karibu kila msimu wa mvua inapofika maisha yao huwa katika hali ya hatari wasijue la kufanya kutokana na mafuriko ya mvua.
Tayari familia 116 zimehama kutoka eneo hilo na kupata makao kwa jamaa zao eneo la Landless na kwingineko. Wakazi hao wanadai mali zao nyingi zimeloweshwa na maji ambayo yaliingia kwa fujo kwenye nyumba zao.
Bw Simon Ngige ambaye ni mkazi wa kijiji hicho alisema: “Wakazi wengi walianza kuhama tangu Jumatano kwa kuhofia maisha yao. Ni hatari kwetu kwa sababu wengi wamelala katika baridi usiku.”
Wakazi walizidi kusema wanaoteseka zaidi ni wanawake na watoto, sasa wanahofia kuzuka kwa maradhi tofauti hasa Malaria, Nimonia na Kipindupindu.
Maeneo kadhaa ya magharibi na kaskazini mwa Kenya pia yanakumbwa na hali sawa na hii ambapo vijiji havikaliki kwa sababu ya mafuriko, huku shule zikigeuzwa kuwa makao mapya ya muda.