Habari Mseto

Wakazi wa Pwani waliojenga katika mikondo ya maji kuhama

December 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

MSHIRIKISHI wa Kanda ya Pwani Bw John Elungata amewaonya wakazi wanaoishi karibu na mikondo ya maji, na akawataka wahamie sehemu salama ili kuepuka kusombwa na maji.

Bw Elungata alisema licha ya serikali kufurusha watu maeneo hayo mwaka jana baadhi ya watu bado wamesalia sehemu hizo.

Alisema baadhi ya watu wamejenga katika njia za maji hivyo kutatiza mtiririko wa maji.

Wiki iliyopita baadhi ya wakazi walisombwa na maji katika kauti za Taita Taveta na Tana River kufuatia mvua kubwa inayoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya Pwani.

“Tumeshuhudia visa vya madaraja kuharibiwa. Mafuriko yamesomba wanyama, watu na hata nyumba. Baadhi ya matukio haya yanatokea kwa sababu watu wamejenga katika njia za maji,” akasema Bw Elungata.

Mwaka 2018 serikali ilibomoa baadhi ya nyumba katika maeneo mbalimbali nchini, ambazo zilidaiwa kuwa katika sehemu za maji.

Aidha aliomba maafisa katika wizara ya ardhi kuhakikisha wanakagua ardhi kuhakikisha ziko salama kabla ya kupeana hati miliki.

“Maafisa katika Wizara ya Ardhi tunaomba mshirikiane nasi kuhakikisha wakazi hawajengi maeneo hatari, Anayenunua pia anapaswa kuwa makini ili kutonunua katika njia za maji,” Bw Elungata akasema.

Kulingana nae maafa mengi ya mafuriko yanatokea kufuatia wakazi kuvamia ardhi zilizoko karibu na bahari,maziwa na mito.

“Nawaomba wakazi ambao wanaishi sehemu zisizo salama kutoka mara moja; heri kupata hasara ya pesa kuliko kupoteza maisha,” akasema Bw Elungata.

Wiki iliyopita Mzee Josphat Maina kutoka eneo la Kokotoni Mariakani alipoteza ng’ombe 15 baada ya ukuta kuwaangukia.

Ukuta huo unasemekana kujengwa katika njia za maji.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Jumapili baada ya mvua kunyesha na kusababisha mafuriko.