Wapuuzeni wanaotumia BBI kujifaidi kisiasa – Mudavadi
WYCLIFF KIPSANG na TITUS OMINDE
KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi, amesihi Wakenya wapuuze baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao anasema wanatumia ripoti ya BBI kupiga siasa za mwaka wa 2022.
Kulingana na Bw Mudavadi, Wakenya wanafaa wapewe muda kusoma na kuelewa ripoti hiyo ili kufanya uamuzi mwafaka.
“Ripoti ya BBI ni hatua mwafaka kwa Wakenya kutoa maoni yao kwa masuala ambayo wanataka yabadilishwe katika katiba. Isitumiwe kuwagawanya Wakenya kwa msingi wa vyama,” alisema Bw Mudavadi.
Alisema hayo Jumapili baada ya kuhudhuria misa katika kanisa la International Vision Centre (IVC) mjini Eldoret .Alieleza kuwa suala la BBI lisitumiwe kupiga siasa za 2022.
Wakati huo huo, Bw Mudavadi alikashifu jinsi gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko alivyozua kioja alipokuwa akitiwa mbaroni kutokana na madai ya ufisadi.
Bw Mudavadi alisema kuwa viongozi wote ambao wanatuhumiwa na madai ya ufisadi wanafaa kuheshimu asasi za serikali na kujisalimisha wakati wowote wanapohitajika.
“Huu ni wakati mwafaka wa nyinyi kusafisha majina yenu. Kama hauna hatia, utaachiliwa,” alisema Bw Mudavadi aliyeandamana na Mbunge wa Lurambi Titus Khamala.