Dhuluma dhidi ya wanawake bado zipo – Umoja wa Mataifa
Na MAGDALENE WANJA
Wakati ulimwengu uliadhimisha siku ya haki za kibinadamu siku ya Jumanne, kitengo cha UN-Women ambacho ni mojawapo ya shirika la Umoja wa Mataifa kilitoa hamasisho dhidi ya baadhi ya haki ambazo zinewaathiri wanawake.
Kulingana na kitengo hicho, dhuluma dhidi ya wanawake haswa kazini zinaendelea kuonekana katika sehemu mbalimbali duniani.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya kitengo hicho, dhuluma hizo zinaweza kuwa moja kwa moja au kwa njipa zingine kwa misingi ya kijinsia.
Kwa njia ambazo sio moja kwa moja kama vile mpango wa pensheni ambao huwafaidi watu ambao hufanya kazi ya kudumu.
Kulingana na UN-Women, kuna idadi kubwa ya wanawake ambao hulazimika kufanya kazi za sulubu.
“Hii huwafanya wanawake hao kutofaidika ama kubaguliwa katika mpango wa pensheni.”
Kitengo hicho pia kilitaja baadhi ya misingi ambayo hutumika kuwabagua watu kama vile mahali pa kuzaliwa, dini, umri, jinsia,ulemavu na kabila.
Taarifa hiyo pia inasema kuwa katika zaidi ya nchi 50 ulimwenguni, wanawake hawaruhusiwi kubadili uraia wao.
“Wanawake hulipwa kiwango cha chini cha mshahara kwa aslimia 23 mapato ya chini kuliko wanaume.”ilisema taarifa hiyo.
Hii imechangia katika umaskini na kuwaweka wanawake katika hatari ya dhuluma.