Habari MsetoSiasa

Giza latanda Nairobi

December 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na COLLINS OMULLO

KAUNTI ya Nairobi sasa iko taabani kufuatia hatua ya mahakama kumpiga breki Gavana Mike Sonko kwenda afisini licha ya kutokuwa na naibu.

Rais Uhuru Kenyatta na madiwani wa Kaunti ya Nairobi sasa ndio wanashikilia ufunguo wa hatima ya jiji la Nairobi.

Sasa kuna mambo matatu: Gavana Sonko kuteua naibu, Rais Kenyatta kuvunjilia mbali kwa muda serikali ya Kaunti ya Nairobi au madiwani kumtimua Bw Sonko na kupisha Spika Beatrice Elachi kuendesha shughuli za serikali ya kaunti.

Tayari majina ya watu watatu yamependekezwa kujaza wadhifa wa Naibu Gavana ulioachwa wazi na Bw Polycarp Igathe aliyejiuzulu Januari mwaka jana.

Duru zilidokezea Taifa Leo kuwa aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru tayari amependekezwa na mrengo wa Kieleweke wa chama cha Jubilee kuwa naibu gavana.

Chama cha ODM kinadaiwa kuwasilisha jina la Katibu Mkuu wake Edwin Sifuna.

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo pia amependekezwa kurithi Bw Igathe.

“Tunachojua ni kwamba Bw Waweru ndiye yuko katika mstari wa mbele katika kinyang’anyiro cha kutaka kuwa gavana kwa mujibu wa mazungumzo ambayo yamekuwa yakiendelea kwa muda mrefu. Upande wa Upinzani pia umewasilisha jina la Bw Sifuna,” akasema mmoja wa watu wamekuwa wakihusika na mazingumzo hayo.

Kulingana na mdokezi huyo, Bw Waweru hapatani na Gavana Sonko hivyo huenda ikawa vigumu kwake kumteua.

Mgawanyiko ulichipuza miongoni mwa madiwani huku Spika Elachi akisema kwamba wataenda likizoni.

Madiwani wa ODM walitaka Spika Elachi kuongeza muda wa vikao vya Bunge .

Madiwani wa upande wa Jubilee walisalia wakipiga kelele: “Hakuna kumtimua Sonko! Hakuna Kumtimua Sonko! Tunajua nia yenu”.