Wezi waogelea katika mafuriko kuibia wahamaji

Na WAANDISHI WETU

WAKAZI wa Rongai, kaunti ya Nakuru wamelalamikia jinsi wezi wanavyotumia wakati huu wa mafuriko kuvunja nyumba na maduka yao na kisha kuiba mali.

Kulingana na wakazi hao ambao sasa wamepiga kambi katika shule za msingi na sekondari za Cesarina, walilazimika kuhama kwenye nyumba zao mnamo siku ya Jumamosi baada ya maji ya mto Rongai kufirika maeneo walikoishi.

Wengi waliondoka ili kuokoa maisha yao na yale ya watoto na kulazimika kuacha baadhi ya mali zao kwenye nyumba na maduka waliyomiliki lakini sasa wezi wanatumia nafasi hiyo kuwaibia.

“Ni jambo la kusikitisha kuona jinsi nyumba zetu na maduka yanavyovunjwa na wezi ambao wanasemekana kuogelea kwenye maji ya mafuriko ili kufika maeneo hayo. Mali nyingi imepotea na hatujui tutasaidika vipi,” akaeleza mmoja wa waathiriwa James Mwangi.

Aliongeza kuwa alishangaa kupata mlango wa duka lake ukiwa wazi siku ya Jumapili huku mali ikiwa imeibwa siku moja baada ya eneo nzima kufurika maji.

Bi Margaret Wanjiku alisema aliporejea nyumbani Jumatatu kuona ikiwa maji yalikuwa yamepungua eneo lao la Burgei, hakupata chochote ndani ya nyumba yake.

Naibu kamishna wa Rongai Bw Julius Kavita aliwasihi wakazi kuwa makini na kuchunga mali yao. Kulingana naye, serikali haitafidia mtu yeyote anayehama na kuacha mali yake katika eneo lililofurika maji.

Naibu huyo wa kamishna alisema kufikia Jumatano, zaidi ya familia 220 zilikuwa zimehamia maeneo salama baada ya makazi yao kufurika.

Maeneo mengine yalioathiriwa pakubwa na mafuriko kwenye kaunti ya Nakuru ni pamoja na Molo, Elburgon na Njoro ambapo wakazi wamekimbilia usalama wao katika shule ya msingi ya Kamara.

Chifu wa eneo hilo Bethwell Kibe alisema familia hizo zitaendelea kupiga kambi katika shule hiyo hadi mvua itakapopungua.

Aliwaomba waathiriwa hao kugawana chochote walicho nacho huku serikali na timu ya wanachama wa msalaba mwekundu ikiendelea kuwasaidia.

Katika Kaunti Ndogo ya Nyatike, Kaunti ya Migori, waathiriwa walikataa kupokea chakula cha msaada kutoka kwa serikali ya kaunti wakisema ni kidogo mno.

Wakiwa wamebeba matawi ya miti, waliandamana katika barabara ya Wath Onger kuelekea Muhuru wakilalamika kwamba maeneo mengine, waathiriwa wa mafuriko wanapokea magunia ilhali wao wanapimiwa posho.

Hayo yametokea huku mtu mmoja akisombwa na maji jana na kuaga dunia alipojaribu kuvuka daraja la mto Rongai karibu na mji wa Salgaa kaunti ya Nakuru.

Mwanamume huyo mwenye umri wa makamu anasemekana kuteleza na kutumbukia katika mto huo mwendo wa saa kumi jioni. Chifu wa eneo hilo la Belba John Njagi, alisema juhudi za kuopoa mwili bado zinaendelea.

Katika Kaunti ya Kisumu, miili miwili inayoaminika ni ya watu waliosombwa na mafuriko ilipatikana ufuoni mwa Mto Wigwe eneo la Nyalenda.

Chifu John Kabisai alisema miili hiyo ya mwanamume na mwanamke haijatambuliwa.

Phyllis Musasia, John Njoroge, Ian Byron Na Elizabeth Ojina

Habari zinazohusiana na hii