Mashabiki wa Spurs wamlia Mourinho kumchezesha Wanyama
Na GEOFFREY ANENE
Mashabiki wa Tottenham Hotspur wamemlia Jose Mourinho kwa kuchezesha kiungo Mkenya Victor Mugubi Wanyama badala ya mshambuliaji kinda Troy Parrot kutoka Jamhuri ya Ireland dhidi ya Bayern Munich katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya, Jumatano.
Mechi hiyo, ambayo Spurs ilipoteza 3-1 uwanjani Allianz Arena nchini Ujerumani, ilikuwa ya kwanza kwa Wanyama chini ya Jose Mourinho tangu kocha huyo Mreno atachukue mikoba ya kunoa Tottenham Hotspur wiki tatu zilizopita.
Huku Spurs ikiwa chini mabao 3-1, mashabiki walitamani sana kuona Parrott akiingizwa kama mchezaji wa mwisho wa akiba.
Hata hivyo, Mourinho alimpatia nahodha huyo wa timu ya Harambee Stars nafasi hiyo katika dakika ya 81. Ilikuwa mechi ya nne ya Wanyama kushirikishwa tangu msimu uanze Agosti 10.
Wachezaji Oliver Skipp na Son Heung-min walikuwa wameingizwa kama nguvu-mpya kujaza nafasi za Giovani Lo Celso na Lucas Moura katika dakika ya 65.
Mourinho alitumia wachezaji kadhaa wachanga kwenye kikosi cha kuanza mechi hiyo akiwemo Ryan Sessegnon aliyeshiriki Klabu Bingwa kwa mara ya kwanza kabisa na kuonyesha uweledi wake wa kuchana nyavu dakika ya 20.
Juan Foyth na Kyle Walker-Peters pia walitumiwa katika safu ya ulinzi. Parrott angeungana na Skipp uwanjani kuchukua nafasi ya mchezaji mwingine wa kutokea akademia ya Tottenham, Eric Dier badala ya Wanyama.
Ingawa ilikuwa mara ya kwanza kiungo wa zamani wa Southampton, Wanyama, kucheza chini ya kocha wake mpya, wawili hawa walikuwa na uhusiano wa aina fulani wa muda mrefu kabla ya kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Manchester United atue Spurs.
Mwaka 2010, Mourinho alinyakua mataji matatu kwa mara yake ya kwanza kabisa akiongoza Inter Milan nchini Italia. Katika kampeni hiyo safi, Mourinho alishinda ubingwa wa Ligi Kuu (Serie A) pamoja na mataji ya Coppa Italia na Klabu Bingwa mjini Milan.
Wakati huo, Diego Milito, Maicon, Samuel Eto’o na Wesley Sneijder walikuwa nyota wa Inter, ingawa pia wachezaji kadhaa walichangia pakubwa katika msimu huo.
Kiungo mkabaji McDonald Mariga alikuwa mmoja waliotoa mchango mkubwa katika ufanisi wa Inter. Yeye hakuwa tu Mkenya wa kwanza kabisa kushiriki Klabu Bingwa Ulaya, bali pia ndiye alikuwa uhusiano wa kwanza na Wanyama, ndugu mdogo wa Mariga.
Mugubi na Mariga wanatoka katika familia ya wanamichezo. Baba yao, Noah Wanyama, alikuwa winga wa pembeni kushoto katika enzi yake kama mchezaji wa timu ya taifa ya Kenya.
Vilevile, kuna ndugu wengine wawili wanaosakata soka katika ligi za Kenya, na dada yao, Mercy Wanyama, anacheza mpira wa vikapu nchini Uhispania.