• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Waiguru amezea mate cheo cha juu

Waiguru amezea mate cheo cha juu

Na NDUNGU GACHANE

GAVANA Anne Waiguru wa Kirinyaga ameeleza nia ya kutaka kushikilia mojawapo ya nyadhifa kubwa katika serikali ijayo, ikiwa mapendekezo ya ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) yatapitishwa.

Kwenye mahojiano ya kipekee na ‘Taifa Leo,’ Bi Waiguru alisema kuwa ikizingatiwa kwamba kutakuwa na Rais, Naibu Rais na Waziri Mkuu, mwanamke anapaswa kuhudumu angaa katika mojawapo ya nafasi hizo.

Bi Waiguru alisema kuwa anaamini ana uwezo wa kuhudumu kwenye mpangilio huo mpya wa utawala ikiwa mapendekezo hayo yatapitishwa na kutekelezwa.

Aliisifu ripoti ya BBI, akisema itahakikisha usawa kwenye uwakilishi wa maeneo mbalimbali serikalini.

“Kuhusu siasa za 2022, ninatathmini nafasi zilizopo. Nitashiriki kwenye mchakato wa maandalizi ya utaratibu wa kubuniwa kwake kwani ninatamani kuchangia katika uongozi wa nchi hii. Ninaamini kwamba nina uwezo wa kuwahudumia watu wetu,” akasema.

“Tunatarajia kwamba tutakuwa na viongozi wawili watakaokuwa manaibu waziri mkuu. Hilo linamaanisha kuwa kutakuwa na nafasi tano kuu katika uongozi wa kitaifa. Ni lazima thuluthi moja ya nafasi hizo itengewe wanawake,” akasema.

Kuhusu siasa za Mlima Kenya, Bi Waiguru alieleza kwamba anaamini atakuwa amejizolea ushawishi wa kutosha katika eneo hilo kufikia 2022, ambao atatumia kuwaraia wakazi kuwachagua viongozi wanaofaa.

“Ninatarajia kuutumia ushawishi wangu kuwarai wanawake kuwania nafasi za kisiasa. Mbali na hayo, nitalishinikiza eneo hilo kuwachagua viongozi wanaofaa,” akasema.

Katika siku za majuzi Gavana Waiguru amekuwa akihusika sana katika shughuli za siasa za Mlima Kenya katika kile kinachojitokeza kuwa mbinu ya kujiweka katika nafasi ya kupata ushawishi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuondoka madarakani 2022.

Hii ni kutokana na kuwa eneo hilo halina kiongozi ambaye amejitokeza wazi kuweza kutoa mwelekeo kwa jamii ya eneo hilo baada ya Rais Kenyatta kung’atuka.

You can share this post!

Wabunge na maseneta wazimwe kuwa mawakili – Uhuru

Kanisa Katoliki lapiga marufuku nguo za kubana mwili...

adminleo