Mwili wa chokoraa aliyezama mtoni akiwa na pingu wapatikana
NA TITUS OMINDE
Mwili wa kijana wa kurandaranda mjini Eldoret ambaye alizama katika mto Sossian akiwa amefungwa pingu umepatikana ukielea.
Anthony Kitango, 23, aliripotiwa kuzama akitoroka polisi ambao walikuwa wamemkamata kwa tuhuma za kuuza dawa za kulevya.
Tukio hilo limeweka polisi lawamani huku jamaa wa marehemu ambaye ni raia wa Uganda pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu wakitaka polisi kuwajibikia tukio hilo.
Polisi wamesisitiza kwamba marehemu aliruka ndani ya mto huo akijaribu kutoroka kutoka kwa maafisa waliokuwa wamemkamata.
Familia yake imepuuza ripoti hio, ikishutumu polisi kwa kusababisha kifo chake.
Monica Watoka ambaye ni dada wa marehemu alisisitiza kwamba kaka yake hakuwa mhalifu inavyodaiwa na polisi
“Polisi lazima waeleze umma kile kilichotokea wakati walipomkamata ndugu yangu,” alisema Bi Watoka
Polisi walichukua mwili huo ukiwa na pingu na kuupeleka katika mochari ya hospitali ya mafunzo ya rufaa ya Moi (MTRH) mjini Eldoret.
Akithibitisha tukio hilo kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Turbo, Eliud Maiyo alikana madai ya familia akisema kwamba marehemu ambaye alikamatwa akiwa na kilo 1.5 za bangi aliruka ndani ya mto uliofurika kutoroka maafisa wa polisi.
“Malalamiko ya familia na watu wa mitaani kwamba polisi walimsukuma ndani ya mto ni ya uwongo. Maafisa wa polisi ni binadamu na hawawezi kufanya kitu kama hicho, “alisema Bw Maiyo.