JAMVI: Ruto atakavyonufaika kwa BBI ikipitishwa

Na LEONARD ONYANGO

RIPOTI iliyotolewa na Jopokazi la Maridhiano (BBI) itamfaa pakubwa Naibu wa Rais William Ruto endapo itatakelezwa jinsi ilivyo.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kuongezwa kwa wadhifa wa waziri mkuu utamfaidi Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Wadhifa huo pia utamsaidia Naibu wa Rais kutegua kitendawili kuhusiana na mwaniaji mwenza wake 2022.

Aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama wiki iliyopita alisema kuwa ataongoza kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kufanya mazungumzo yanayolenga kuunda muungano wa kisiasa na Dkt Ruto kwa ajili maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Bw Muthama aliwapongeza wabunge kutoka maeneo ya Ukambani; Victor Munyaka (Machakos Mjini) na Vincent Musyoka (Mwala), huku akisema kuwa atahakikisha kuwa Bw Musyoka anapata wadhifa kwenye serikali ijayo.

Bw Musyoka, hata hivyo, amejitenga na kauli hiyo ya Bw Muthama huku akisema kuwa ni njama ya kutaka kusambaratisha uhusiano mwema baina yake na Rais Uhuru Kenyatta.

“Kumekuwa na madai kwamba nashirikiana na Naibu wa Rais. Napenda kuwafahamisha kwamba madai hayo ni njama inayolenga kunitenganisha na Rais Kenyatta. Kauli zinazotolewa na watu binafsi hazifai kuhusishwa na mimi,” akasema Bw Musyoka kupitia mtandao wa Twitter.

Bw Musyoka, wiki iliyopita, alikutana na Rais Kenyatta kwenye Ikulu ya Nairobi katika kile wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa ilikuwa kumwakikishia kuwa hakuna mazungumzo ya siri baina yake na Naibu wa Rais.

Aliyekuwa mwaniaji wa ugavana wa Kaunti ya Machakos Wavinya Ndeti anadai kuwa wanaohusisha Bw Musyoka na Naibu wa Rais wanafadhiliwa na Gavana wa Machakos Alfred Mutua ili watenganishe kinara wa Wiper na Rais Kenyatta.

“Hakuna mazungumzo yanayoendelea baina ya kiongozi wa chama chetu na naibu wa rais. Wanaotoa madai hayo wana njama fiche. Msimamo wa chama cha Wiper ni kwamba tunaunga ripoti ya BBI pamoja na vita dhidi ya ufisadi,” Bi Ndeti akaambia Taifa Jumapili.

Cheche za maneno katika siku za hivi karibuni baina ya kiongozi wa Amani National Alliance (ANC) Musalia Mudavadi na kinara wa ODM Raila Odinga ni ishara kwamba wawili hao hawatashirikiana kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao.

“Hivyo, Bw Mudavadi amesalia na mambo mawili; kuungana na Naibu wa Rais Dkt Ruto au kuwania urais akiwa pekee kama alivyofanya katika uchaguzi wa 2007. Akiungana na Dkt Ruto atakuwa na nguvu za kisiasa na akiwania pekee yake ataambulia patupu,” anasema wakili Felix Otieno.

Wakili Otieno, anasema kuwa kwa kutumia wadhifa wa waziri mkuu uliopendekezwa katika ripoti ya BBI, Dkt Ruto anaweza kuwanasa Bw Mudavadi na Bw Musyoka kwa mpigo.

“Dkt Ruto anaweza kumteua Bw Musyoka kuwa mwaniaji wake mwenza na kisha Bw Midavadi kuwa waziri mkuu. Hapo atakuwa amejipatia ushawishi katika maeneo ya Magharibi, Ukambani pamoja na ngome yake ya Bonde la Ufa na kaunti za jamii za wafugaji,” anasema.

“Ikiwa ripoti ya BBI haitatekelezwa na twende kwenye uchaguzi na Katiba jinsi ilivyo, Naibu wa Rais atakuwa na mwaniaji mwenza pekee. Kwa mfano, akiteua Bw Musyoka kuwa mwaniaji wake, atakuwa amepoteza maeneo ya Mlima Kenya na Magharibi hivyo itakuwa vigumu kwake kushinda uchaguzi wa 2022,” anaongezea.

Tayari Naibu wa Rais ameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa ripoti ya BBI inapitishwa jinsi ilivyo bila kufanyiwa mabadiliko.

Awali, Naibu wa Rais pamoja na wanasiasa wanaomuunga mkono wa mrengo wa Tangatanga, walikuwa wameapa kupinga ripoti ya BBI endapo ingependekeza kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka.

Tayari Naibu wa Rais ameunda vikosi vya kimaeneo ambavyo vitamsaidia kushinikiza ripoti ya BBI kupitishwa jinsi ilivyo bila kufanyiwa mabadiliko.

Kundi la Mlima Kenya linaoongozwa na Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri na lilifanya mkutano wake wa kwanza katika Kaunti ya Embu wikendi mbili zilizopita.

Kundi la eneo la Nakuru linaoongozwa na mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri.

Wandani wa Ruto kutoka Kaunti za Isiolo, Marsabit na Samburu pia walikutana kujadili ripoti ya BBI.

Wanasiasa wa kundi la Tangatanga wanasema kuwa wanaunga ripoti ya BBI na wanataka itekelezwe kupitia Bungeni au kura ya maamuzi.

Hatua ya Rais Kenyatta kuongezea muda jopokazi la BBI kuhakikisha kuwa ripoti inatekelezwa kikamilifu, imezua hali ya suitafahamu katika kambi ya Tangatanga.

“Tunangojea Rais achapishe taarifa ya kuongezea muda jopokazi la BBI kwenye Gazeti Rasmi la Serikali. Ni kupitia gazeti hilo ambapo tutajua mambo ambayo wanakamati 14 wa BBI wanalenga kutekeleza,” akasema mbunge ambaye ni mwandani wa Naibu wa Rais aliyeomba jina lake libanwe.