Wenye matatu sasa wageukia ndumba kuvuta wateja
Na STEPHEN ODUOR
WAMILIKI wa matatu katika Kaunti ya Tana River wamelaumiana kuhusu utumizi wa juju kuvutia wateja na kuharibia wenzao riziki.
Ndumba ambazo zimekuwa zikitumiwa kwa muda mrefu na wanasiasa na wafanyabiashara wengine sasa zimeingia katika sekta ya matatu huku wamiliki wakitaka utajiri wa haraka.
Mmiliki wa matatu, Yusuf Ijema ambaye alihudumia barabara ya Garsen-Malindi alikuwa ameleta gari jipya katika kituo ambacho kilikuwa na magari makuukuu na hivyo abiria wakawa wanapenda zaidi gari lake.
Lakini wakati mmoja, gari likapata ajali kwa njia zisizoeleweka na uvumi ukaenezwa kwamba alitoa watu kafara. Muda mfupi baadaye, gari tena likagonga ng’ombe barabarani.
Hapo ndipo alipoenda kwa mganga ambaye alimfichulia kwamba kuna wamiliki wengine wanne wa matatu ambao hutafuta huduma kwake kulinda biashara zao. Lakini anasema hakutaka huduma za mganga kwa kuwa yeye ni muumini Muislamu.
Katika mahojiano na Taifa Leo, mganga almaarufu ‘Daktari’ alikiri kuwa ana wateja wengi wanaojumuisha wafanyabiashara, wanasiasa na wazazi wanaotaka watoto wao wapite mitihani.
“Msidanganyike na zile rozari ambazo nyinyi huziona zikining’inia katika matatu. Nyingine zina hitilafu, wakati mwingine huyo Yesu huwa hana mkono mmoja au kichwa chake si cha kawaida,” akasema, akifichua kwamba nyingi huwa ni za ushirikina.
Mmiliki mwingine, Bw Samuel Baya anayehudumu kwenye barabara ya Hola-Malindi-Mombasa alisema alipotishiwa kuhusu uchawi, alidhani ni utani.
Biashara yake ilianza vyema hadi wakati washindani wapya walipoingia.
“Siku moja baada ya kujaza abiria kwenye gari langu tukawa karibu kuondoka, gari lilikataa kuwaka. Tulijaribu kila tuwezalo, tukaita mekanika ambaye alilikagua kwa saa moja na hakupata hitilafu yoyote,” akasema.
Wakati huo, gari la mshindani wake lilikuwa limeegeshwa likiwa na dereva pekee, wala hapakuwa na manamba aliyemwitia abiria.
Ghafkla bin vuu wasafiri waliokuwa katika gari lake walichoka, wakashuka na kudai nauli waliyokuwa wamelipa na hapo ndipo mshindani wake akawaita na gari lake likaondoka mara moja. Baada ya dakika 20, gari lake liliwaka lakini sasa asingeweza kupata wateja wa kutosha.