• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
Wanakijiji walia mvua kubwa kuharibu mali

Wanakijiji walia mvua kubwa kuharibu mali

NA LAWRENCE ONGARO 

WAKAZI wa kijiji cha Kiganjo Thika, wanalalamika hasara baada ya mvua kubwa kuharibu mali yao.

Walisema kwa zaidi ya wiki moja sasa biashara zao zimeathirika kwa sababu ya maji yaliyofurika maeneo hayo.

Mbunge wa Thika, Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alisema mafuriko hayo pia yaliweza kushuhudiwa mwaka jana wa 2018.

“Nikiwa mbunge wa eneo hili nitafanya juhudi kuona ya kwamba maji taka yanaondolewa ili kuruhusu maji ya mvua kupata mwanya wa kusambaa,” alsema Bw Wainaina.

Alisema wakazi wa Kiganjo ni wenye bidii ya biashara na kwa hivyo wanatoa ushuru ya juu katika idara ya KRA.

Aidha alisema ni vyema kuona ya kwamba barabara za sehemu hiyo zinaundwa kwa utaratibu ufaao.

Alisema mwaka jana afisi yake ilikarabati barabara ya kuingia eneo hilo la Kiganjo lakini baadaye mvua iliyonyesha juzi iliharibu eneo hilo lote.

“Hata hivyo nitafanya juhudi kuona ya kwamba barabara hiyo inarekebishwa kwa manufaa ya wakazi hao. Tayari usafiri imekuwa ni shida kubwa,” alisema mbunge huyo.

“Nitafanya juhudi kuona ya kwamba mabwawa yanayoweza kuhifadhi maji siku za usoni yanaundwa kwa manufaa ya wakazi hao,” alifafanua.

Bi Ruth Njeri mkazi wa Kiganjo alisema biashara katika eneo hilo imeathirika sana kwa sababu karibu eneo lote limefurika kabisa.

“Sisi wakazi wa hapa tunahofia kuzuka kwa maradhi ya malaria na kolera na hata kufurika kwa maji taka,” alisema Bi Njeri na kuongeza kaunti ya Kiambu inastahili kuingilia kati ili kurekebisha hali hiyo.

Alisema wakazi wengi wanalazimika kushinda ndani ya manyumba zao kwa sababu kila sehemu imezungukwa na maji machafu.

Bi Regina Ndunge ambaye pia ni mkazi wa kijiji hicho anasema watoto wengi wako katika hatari ya kuambukizwa maradhi tofauti kwa sababu ya kucheza na maji taka yanayosambaa kila mahali.

“Hata hivyo wakazi wengi majuzi walikosa kuhudhuria ibada ya kanisa kwa sababu hakuna njia kamili ya kupitia,” alisema Bi Ndunge.

Alisema iwapo hatua ya haraka haitachukuliwa bila shaka wafanyi biashara wengi watapata hasara kubwa .

Peter Kimani ambaye ni muhudumu wa bodaboda anasema kwa zaidi ya wiki moja sasa wamekosa wateja wa kubeba kutokana na hali mbaya ya mazingira.

“Wakazi wengi wanalazimika kutembea juu ya maji hayo ili kuepuka kuanguka wakibebwa na bodaboda. Wateja wetu wameogopa kupanda bodaboda wakidai wataanguka kwenye maji,” alisema Bw Kimani.

You can share this post!

Wakazi wafurahia ujenzi wa barabara

Nitaangamiza ufisadi Kiambu, aapa Nyoro

adminleo