• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:15 AM
Korti kuamua iwapo Rais atashurutishwa kuwaapisha

Korti kuamua iwapo Rais atashurutishwa kuwaapisha

Na Richard Munguti

MAJAJI 41 walioteuliwa kujiunga na Mahakama ya Rufaa na Mahakama za kuamua kesi za mashamba na mizozo ya wafanyakazi, watajua hatma yao Februari 6, mwaka ujao.

Hatma yao itajulikana majaji watatu watakapoamua iwapo watamshurutisha Rais Uhuru Kenyatta kuwateua na kuwaapisha.

Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) , jana iliwaambia Majaji Lydia Achode, Enoch Chacha Mwita na James Makau, kwamba “Rais hana budi ila kuwaapisha majaji iliyowateua.”

Majaji 41 waliteuliwa Julai mwaka huu lakini kukawa na kizingiti baada ya idara ya ujasusi kusema baadhi yao walikuwa na dosari.

Kupitia kwa wakili Paul Muite, JSC pamoja na mwenyekiti wake, ambaye pia ni Jaji Mkuu David Maraga, aliambia majaji hao kuwa, Rais Kenyatta anatakiwa kikatiba kuwateua majaji hao ambao majina yao yaliwasilishwa kwake bila kusita.

“Itambidi Rais Kenyatta awateue majaji aliopelekewa na JSC baada ya kuhojiwa na kupatikana wamehitimu. Kisheria hawezi kuanza uchunguzi mwingine baada ya JSC kukamilisha jukumu lake,” alisema Bw Muite.

Alisema JSC iliomba ushahidi iwapo kuna malalamishi dhidi ya majaji hao 41 lakini hayakutolewa .

“Katiba iko wazi kwamba JSC ikisha wateua majaji, Rais hana mamlaka ya kuzindua upya uchunguzi ama upekuzi mwingine kwa vile huwa imekamilisha jukumu lake,” alisema Bw Muite.

Wakili huyo alisema “JSC kupitia kwa katibu wake ambaye pia ni Msajili wa Idara ya Mahakama, Bi Anne Amadi iliandikia Idara ya Ujasusi nchini (NSIS) ikiomba ijulishwe iwapo majaji hao walikuwa na dosari.”

Kwa mara ya kwanza, NSIS ilisema haikuwa na chochote dhidi ya majaji ambao majina yao yalipelekwa Rais awateue.

Bw Muite alisema kuna maamuzi ya awali kwamba Rais hana budi ila kuwateua majaji waliopendekezwa kujiunga hizo.

Wakili huyo aliwaomba Majaji hao watatu wakubalie ombi la JSC na wakili Adrian Kamotho kwamba Rais awateue majaji hao 41 na kuwaapisha waanze kutekeleza kazi zao mara moja.

Lakini wakili huyo alimshutumu Mwanasheria Mkuu kwa kuzembea kazini alipokosa kumwita Mkurugenzi wa NSIS kumtaka aipe JSC ushahidi wa majaji aliodai ni wafisadi.

You can share this post!

Waiguru atishia kumshtaki King Kaka kuhusu wimbo wa...

Maimamu wataka tume mpya ibuniwe kusaidia EACC

adminleo