• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
#WajingaNyinyi: BBI kuwalinda wanaoanika mafisadi

#WajingaNyinyi: BBI kuwalinda wanaoanika mafisadi

Na LEONARD ONYANGO

RIPOTI ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) inalinda watu wanaokemea maafisa wafisadi dhidi ya kushtakiwa.

Hii inatoa afueni kwa wakosoaji wakiwemo wanahabari, wasanii na wanaharakati wanaolalamikia ufisadi miongoni.

Ripoti hiyo inapendekeza kuwa sheria inayoadhibu watu wanaochafua sifa za wengine kwa kudai ni wafisadi ifanyiwe mabadiliko ili kulinda wakosoaji.

“Sheria hiyo ibadilishwe ili maafisa wa serikali wasiwashtaki wanahabari au watu wanaofichua au kukemea sakata za ufisadi na masuala mengineyo ya kimaadili,” inasema ripoti ya BBI.

Licha ya kuunga mkono ripoti ya BBI, Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru ametoa makataa ya saa 48 kwa mwanamuziki Kennedy Ombima, maarufu King Kaka, kuondoa katika mtandao wa YouTube wimbo wa ‘Wajinga Nyinyi’.

Wimbo huo umehusisha Bi Waiguru na sakata ya wizi wa mamilioni ya fedha katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS).Ga

vana huyo, kupitia kwa kampuni ya mawakili ya Kiragu Wathuta, anasema wimbo huo umemchafulia sifa.

Bi Waiguru ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamekuwa wakipigia debe ripoti ya BBI iliyozinduliwa Novemba 26, mwaka huu, katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

King Kaka alienda katika makao makuu ya Idara ya Kuchunguzi Uhalifu (DCI) akidai alikuwa ameitwa kuhojiwa.Lakini Idara ya DCI ilikataa kuandikisha ripoti kutoka kwake ikisema haikuwa imemuita.

King Kaka alisisitiza alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama Callen Onyancha akimtaka kufika katika idara ya DCI.Mawakili Ahmednasir Abdullahi na Nelson Havi wametangaza kuwa watamwakilisha mwimbaji huyo kortini bila malipo iwapo atashtakiwa.

“Niko tayari kumwakilisha King Kaka mahakamani. Wanaomshtaki watakuwa na wakati mgumu na watalipia kesi hiyo kwa kuwa watashindwa,” akasema Bw Havi.Naye Bw Abdullahi alisema: “Nitamwakilisha King Kaka dhidi ya yeyote atakayethubutu kumshtaki.”

You can share this post!

Sonko kujibu mashtaka mapya Voi

ODONGO: Tuangazie utendakazi wa Raila, Ruto kuliko asili yao

adminleo