Kasisi motoni kwa kualika Tangatanga kwa harambee
Na KNA
KASISI wa Kanisa Katoliki mjini Bondo, Kaunti ya Siaya amejipata mashakani baada ya kualika wandani wa Naibu Rais William Ruto katika harambee ambayo haikuhudhuriwa na mwanasiasa yeyote wa Chama cha ODM kilicho na ufuasi mkubwa eneo hilo.
Uvumi sasa umeanza kuenea kwamba viongozi wa Kanisa Katoliki la St Andrews eneo la Bondo, ni wanachama wa vuguvugu la Tangatanga.
Waumini wa kanisa hilo wanaamini kwamba, uvumi huo unaenezwa na wanachama wa ODM waliokasirika wakubwa wao walipokosa kualikwa katika harambee iliyofanyika Parokia hiyo majuzi.
Viongozi walianza kurushiana lawama punde tu baada ya msaidizi wa Naibu Rais William Ruto- Bw Farouk Kibet, kiongozi wa wengi katika seneti Kipchumba Murkomen na aliyekuwa mgombeaji wa chama cha Jubilee kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra Macdonald Mariga- walipohudhuria harambee katika kanisa hilo mapema mwezi huu.
Kuhudhuria kwa watatu hao wanaochukuliwa kuwa “wageni” na kukosekana kwa viongozi wa eneo hilo katika harambee hiyo kulimweka pabaya Kasisi Collins Odiero huku ripoti zikienea kuwa aliwapuuza makusudi viongozi wa ODM na kuwaalika wale wa Jubilee.
Uvumi huo ungali unaendelea tangu Desemba 1 wakati harambee ilifanyika na Sh6.5 milioni kukusanywa kujenga afisi za Parokia.
Baadhi ya wakazi wanadai kuwa, viongozi wa kanisa wangewaalika viongozi wa vyama vyote huku baadhi wakimuunga Padre Odiero wakisema aliwaalika waliokuwa tayari kuchanga pesa.
“Tuna wandani wa viongozi wa ODM miongoni mwa waumini. Tafadhali komeni kutupiga vita kutoka ndani mliposhindwa kutujulisha kwa wakubwa wenu tulipowahitaji,” Padre Odiero alisema kwenye ibada Jumapili.
Alisema kamati iliyoandaa harambee ilijaribu kuwafikia viongozi wakuu wa ODM eneo hilo kwa miezi minne kupitia wandani wao na hata kwa kuwapigia simu lakini hakuna aliyekubali.
“Siku chache kabla ya harambee, tuligundua hawangefika,” alisema Padre Odiero.
Alisema yeye binafsi alimuita diwani ambaye pia ni mshirika wa kanisa lakini hakujitolea kuwaalika na hata mwenyewe hakuhudhuria.
Kwa vile muda ulikuwa unayoyoma, kamati iliamua kuwasiliana na msaidizi wa Dkt Ruto, ambaye ni Bw Kibet, na akakubali mara moja kuwa mgeni wa heshima.
“Kusema ukweli, sikufahamu kwamba Bw Kibet angeandamana na Murkomen na Mariga lakini walituchangia zaidi ya Sh800,000 kusaidia kujenga kanisa na hakuna shida yoyote. Sisi sio wanasiasa na hatuhusiki na siasa,” alisema Padre Odiero.
Aliwataka wafuasi wa ODM wanaoabudu katika kanisa hilo kukoma kueneza uvumi kwa nia mbaya ili kumchafulia jina kama msimamizi wa Parokia.
Lakini afisa wa ODM Peter Mbeka, ambaye kanisa lilisema lilimtumia kuwasiliana na Seneta Orengo amekanusha kueneza uvumi na kugawanya kanisa.
Alikiri kwamba alitwikwa jukumu la kuwasiliana na Bw Orengo lakini kamati ilipotakiwa kuandika barua ilikataa.
Alifichua kuwa wakati wa harambee aliwasiliana na mbunge wa eneo hilo Dkt Gideon Ochanda ambaye alituma mchango wake kupitia Bw Kibet.