Habari Mseto

Magoha sasa kukaza kamba CBC

December 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

BAADA ya kuridhishwa kwamba mageuzi ya usimamizi wa mitihani ya kitaifa yanazaa matunda, sekta ya elimu sasa inaelekeza macho yake kwa utekelezaji wa Mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC).

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha jana alisisitiza wizara yake itaendelea kutoa mafunzo kabambe kwa walimu ambao wanatekeleza jukumu muhimu la kuutekeleza.

Alisema kuwa awamu ya masomo ya gredi ya nne itazinduliwa Januari 13 kote nchini na akawahakikishia wazazi kwamba vitabu vyote vya darasa hilo vimesambazwa katika shule zote.

“Mwaka ujao tutawapa mafunzo walimu ambao watakuwa wanafundisha mtaala wa CBC. Pia hakutakuwa na mtihani kwenye gredi ya sita jinsi ilivyoamuliwa mwaka huu. Tutaendelea kuhakikisha CBC inafaulu na wanaotatiza utekelezaji wake wanafaa kujiunga nasi kuufanikisha,” akasema Prof Magoha katika Jumba la Mtihani jijini Nairobi.

Vilevile alishikilia kwamba mbinu ya kiteknolojia ya kuwatambua wanafunzi maarufu kama Nemis utaendelea kutumika, akikanusha kwamba serikali imerejelea mfumo wa zamani wa kuwahesabu wanafunzi moja kwa moja.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) Dkt Nancy Macharia naye aliwatambua walimu Peter Tabichi na Peter Ademba ambao walijizolea tuzo za kimataifa kutokana na utendakazi wao mzuri kwenye shule zao.

Dkt Macharia pia alitangaza kwamba tume yake itawaajiri walimu 10,000 kwa kandarasi ili kusaidia kukabiliana na upungufu wa walimu katika shule za upili kote nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mtihani Nchini(KNEC) John Onsati pamoja na Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji Dkt Mercy Karogo walishikilia kwamba wataendelea kuwajibika kuhakikisha kwamba mitihani ya kitaifa inaendeshwa kwa uwazi bila udanganyifu.