KCSE 2019: Wasichana waendelea kuandikisha matokeo bora
Na CHARLES WASONGA
KWA mara nyingine wasichana waliandikisha matokeo mazuri katika mtihani wa kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka huu.
Hata hivyo, kwa ujumla, wavulana walifanya vizuri zaidi kuliko wasichana huku Buluma Tony Wabuko wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Kapsabet akiibuka bora zaidi kitaifa kwa kupata alama wastani ya 87.159.
Wasichana watano walikuwa miongoni mwa watahiniwa 10 bora ambapo Barasa Maryanne Njeri wa Shule ya Upili ya Kenya High alikuwa wa pili kwa kupata alama 87.087.
Natasha Wawira wa Kenya High alikuwa wa tano bora kwa kupata alama ya wastani ya 86.1 huku mwenzake Ndathi Hellen Njoki akishilikia nafasi ya nane kwa alama 86.914.
Nambari tisa alikuwa Siele Chelang’at Aillen wa Moi Forces Academy, Lanet aliyepata alama 86.9 huku Laura Chelagat wa St Brigd, Kiminini akifunga orodha ya hiyo ya 10 bora kwa alama 86.
Katika tapo la Shule 10 bora kwa misingi ya idadi ya watahiniwa waliopata alama ya A, shule tatu za wasichana ziliorodheshwa. Shule hizo Alliance Girls (A, 27), Mary Hill iliyopata ‘A’ 25 na Moi Girls, Eldoret iliyoandikisha alama 21 za A.
Kulingana na matokeo hayo yaliyotolewa jana na Waziri wa Elimu George Magoha, watahiniwa wa kike waliwashinda wenzao wa kiume katika masomo ya lugha za Kiingereza, Kiswahili na Kijerumani, Somo la Dini ya Kikristo (CRE), Sayansi ya Nyumbani (Home Science), Sanaa na Uchoraji na Lugha ya Ishara.