• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
‘Nidhamu ilitusaidia kuwika KCSE’

‘Nidhamu ilitusaidia kuwika KCSE’

Na LAWRENCE ONGARO

SHULE ya upili ya MaryHill Girls’ High, Kiambu imesema inajivunia ufanisi kutokana na nidhamu, kumcha Mungu, na kujituma masomoni.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi Jecinta Waweru Ngure alisema wanafunzi wapatao 337 ndio walifanya mtihani huo ambapo 333 wanatarajiwa kujiunga na chuo kikuu.

Alisema wanafunzi 25 waliofanya mtihani wa KCSE mwaka wa 2019, waliandikisha alama A huku 117 walipata alama A-. Wanafunzi 89 waliandikisha B+. 54 walipata B, 26 wakapata B- , 16 walikuwa na C+, huku 4 wakiandikisha C-.

Alisema walimu katika shule hiyo walikuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba wanafunzi wanazingatia masomo yao bila kulegea.

“Wanafunzi hao walijituma wenyewe kwa kusoma kwa bidii huku wakirauka usiku wa manane kujisomea wenyewe na pia kujiamini katika masomo yao,” alisema Bi Ngure.

Shule hiyo ilikuwa miongoni mwa sita bora katika nchi nzima, huku akipongeza wazazi kwa ushirikiano mkubwa waliokuwa nao na wana wao pamoja na walimu.

Mwanafunzi wa kwanza Verra Karimi alipata alama A na pointi 84 na alimshukuru Mungu kwa kumwezesha kuongoza shule nzima.

“Ama kwa kweli sitaki kuwasahau walimu wangu wapendwa ambao walikuwa mstari wa mbele kila mara kututia shime kusoma kwa bidii,” alisema binti Karimi.

Alipongeza juhudi za wazazi wake kwa kumwezesha kufika kiwango hicho kwa kumfanyia matakwa yote aliyoulizia.

“Haikuwa kazi rahisi kwa sababu tulikuwa tukirauka mapema kujisomea wenyewe lengo letu likiwa ni kupita mtihani huo bila wasiwasi,” alifafanua

Alisema azma yake kuu kwa sasa ni kusomea uhandisi wa kujenga majumba (Architect), kwa sababu anapendezwa na kuona jinsi majumba makubwa yanavyojengwa.

Mwanafunzi mwingine aliyepata alama A Deisy Wanjiru Kuria alipata alama 81 anasema lengo lake kuu ni kuwa Daktari wa upasuaji na saratani.

Anasema licha ya wazazi wake kutoka katika familia ya wakulima wa majani chai bado alijikakamua na kufanya vyema katika mtihani wake.

“Mimi nawashukuru wazazi wangu kwa kunipa moyo wa kusoma kwa bidii. Kila mara walinihimiza kujikakamua kwa masomo bila kurudi nyuma,” alifafanua Wanjiru.

Waaaaanafunzi wengine waliofanya vyema na alama za juu ni Anne Wairimuy Nduati, na Pacient Mutua ambao wote wanafurahia kwenda chuo kikuu.

Padri wa kikatoliki Father Julius Nyandiga wa shirika la passionate Congregation alisema maombi ya kila mara yalikuwa jawabu kuu ya wasichana hao kupita na alama za juu.

“Tumekuwa tukiwapa mawaidha ya kila mara jinsi ya kuwa na maadili mema maishani na kufanya bidii masomoni,” alisema Padri Nyandiga.

You can share this post!

Huenda Wanyama akayoyomea China

Kiungo chipukizi anayelenga kusakata soka Stamford Bridge

adminleo