Habari Mseto

Watahiniwa walemavu waongezeka, wang’aa

December 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MARY WANGARI

JUMLA ya watahiniwa 1,672 wenye ulemavu walishiriki Mtihani wa Kitaifa kwa Shule za Upili (KCSE) mwaka huu miongoni mwa wanafunzi 667,222 waliofanya mtihani.

Idadi hiyo iliongezeka pakubwa ikilinganishwa na wanafunzi 1,499 wenye ulemavu waliofanya mtihani huo mwaka uliopita, kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumanne, kutoka kwa Waziri wa Elimu Profesa George Magoha.

Isitoshe, kulingana na taarifa hiyo, idadi kubwa ya watahiniwa hao walemavu ilijumuisha wanafunzi wenye ulemavu wa viungo ambapo 651 walishiriki mtihani huo wa kitaifa.

Katika kundi hilo la watahiniwa wenye ulemavu, wanafunzi wanne walijizolea alama ya A- (minus) huku wanafunzi zaidi ya 100 wakijikakamua kujitwalia alama ya C+ (plus) kuenda juu.

“Wanafunzi wanne katika kitengo hiki walipata alama ya A- (minus) huku 127 wakipata alama ya C+ kuenda juu.”

“Ni dhahiri kwamba, wakipewa mazingira mazuri, wanafunzi wenye mahitaji ya kipekee wanaweza kufanya vyema katika mitihani,” ilisema taarifa hiyo.

Wanafunzi 667,222 walishiriki mtihani huo wa KCSE mwaka huu kote nchini ambapo watahiniwa 355, 782 sawa na asilimia 51, walikuwa wavulana huku watahiniwa 341,440 ambayo ni asilimia 48, wakiwa wasichana, hivyo kukaribia usawa katika jinsia.

Kuhusiana na jinsia, watahiniwa wa kike kwa jumla waliandikisha matokeo bora kushinda wenzao wa kiume katika mtihani wa KCSE mwaka huu.

Wanafunzi wasichana waliwabwaga wavulana katika masomo manane ikiwemo: Kiingereza, Kiswahili, Somo la Dini ya Kikristo (CRE), Sayansi Kimu, Sanaa na Ufundi, Kijerumani na Lugha ya Ishara Kenya.