Habari Mseto

Makanga wamsaidia mjamzito kujifunga katika steji

December 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na KANYIRI WAHITO

MAKANGA wa mabasi ya kampuni ya Embassava jijini Nairobi mnamo Ijumaa jioni walimsaidia mwanamke mjamzito kujifungua alipozidiwa na uchungu kituoni.

“Niliona tu mwanamke akizunguka kwa uchungu kabla ya kupiga magoti huku mumewe aliyekuwa amebeba mkoba akijaribu kumsimamisha. Ghafla alipiga usiahi na mtoto akatoka. Kwa bahati nzuri niliweza kufika kwa wakati kushika kichwa cha mtoto alipokuwa akitoka,” alisimulia Bw Joseph Anari, mhudumu wa matatu katika kituo hicho cha mabasi.

Wahudumu wa mabasi ya Embassava ambao wengi wao ni wanaume, walikimbia kumsaidia mwanamke huyo huku wakimpa koti ili amfunike mtoto na kuwaita wapita-njia wanawake kumpa usaidizi.

Mwanamke mmoja alitoa kikuba chake na kukitumia kufungia kitovu cha mtoto huku wahudumu wa Embassava wakizuia magari na mmoja wao akakimbilia teksi karibu na makavazi ya kitaifa.

Pindi teksi hiyo ilipopita, wanawake walimzingira mama huyo na mtoto wake mchanga alipokuwa akiingizwa kwenye teksi na kukimbizwa katika hospitali ya kujifungulia akina mama ya Pumwani.

Taifa Leo ilipozungumza kupitia simu na baba huyo (jina limebanwa) alithibitisha kuwa bintiye na mke wake walikuwa salama na alikuwa akiwashughulikia ili waweze kuruhusiwa kwenda nyumbani.

“Niliondoka Ruiru nikitumai kumpeleka mke wangu katika Hospitali ya Pumwani lakini akajifungua tulipokuwa tukielekea katika kituo cha mabasi ya kwenda mtaani Eastleigh,” akasema mume huyo.

Alisema mtoto na mama yake wanaendelea vyema. Bw Anari alisema alimshukuru Mungu kwa kushika kichwa cha mtoto alipozaliwa.

“Wazazi wake walinieleza wanafikiria kumpa mtoto jina langu,” alisema huku akitabasamu.