Ruto akutana na Abagusii, Abaluhya na Agikuyu kujipanga 2022
Na WAANDISHI WETU
NAIBU Rais William Ruto wiki hii alikutana na jumbe kadhaa, kutoka maeneo mbalimbali nchini, nyumbani kwake eneo la Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu kwenye mikakati ya kujijenga kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2022.
Dkt Ruto alipokea jumbe kutoka jamii za Abagusii, Abaluhya na Agikuyu wanaoishi katika eneo la Bonde la Ufa.
Kwa miaka mitatu iliyopita, Dkt Ruto amekuwa akitumia mbinu hiyo kupokea jumbe zinazowajumuisha madiwani, wabunge na viongozi wa kidini hasa katika msimu wa Desemba.
Mabasi ya shule mbalimbali yalionekana yakielekea nyumbani kwake, kuwasafirisha wageni wake.
Duru ziliieleza kwamba Dkt Ruto amekuwa akitumia mikutano hiyo kujipigia debe kuhusiana na uchaguzi wa 2022. Vilevile, amekuwa akiwaeleza kuhusu mikakati ya maendeleo atakayoweka.
Wiki hii, Dkt Ruto alikutana na jumbe tatu tofauti kutoka eneo la Magharibi. Mnamo Jumatatu, alikutana na viongozi wa kisiasa kutoka Bungoma, ambao waliandamana na viongozi wengine zaidi ya 1,000 wa mashinani.
Mnamo Jumatano, alikutana na ujumbe mwingine kutoka Kaunti ya Kakamega, uliowashirikisha watu 1,400.
Mnamo Ijumaa, alikutana na viongozi kutoka Kaunti ya Busia, ambao waliandamana na watu 500.
Anatarajiwa kukutana na ujumbe mwingine kutoka Kaunti ya Vihiga, lakini bado haijabainika yale yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo. Ingawa waliohudhuria mikutano hiyo walisema iliangazia masuala ya maendeleo katika eneo la Magharibi, baadhi yao walisema kuwa Dkt Ruto anaitumia kuandaa mikakati ya kisiasa.
“Malengo yetu kama viongozi waliochaguliwa na wale ambao hawajachaguliwa katika eneo hilo ni kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imefadhiliwa na serikali. Baadhi ya miradi hiyo imekwama huku mingine ikiwa bado haijaanza kutekelezwa,” akasema aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Dkt Bonny Khalwale.
Akaongeza: “Tumeamua kusimama na Naibu Rais kama jamii kwani amedhihirisha kwamba anajali maslahi yake na ataifanyia mengi ikiwa atatwaa urais.”
Baadhi ya ripoti zimeeleza kuwa Dkt Ruto atabuni muungano wa kisiasa na kiongozi chama cha ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula katika uchaguzi huo.
Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, aliye mshirika wa karibu wa Dkt Ruto alipuuzilia mbali madai kwamba mikutano hiyo ni ya kisiasa.
Ripoti za Wycliffe Kipsang, Dennis Lubanga, Ruth Mbula na Benson Amadala