Jinsi ya kuwa salama wakati huu wa Krismasi

Na MWANDISHI WETU

Katika msimu wa Krismasi, watu wengi huzingatia sana sherehe na kusahau usalama wao na mali yao.

Hata hivyo, mtaalamu wa masuala ya usalama, Tony Sahni, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya usalama ya Securex anatoa mwongozo ambao watu wanapaswa kutumia kujihakikishia usalama wao, watoto na mali yao.

Bw Sahni anatahadharisha watu dhidi ya kutangaza mahali walipo msimu huu katika mitandao ya kijamii akisema habari hizo zinaweza kutumiwa na wahalifu kuwalenga.

“Wakati kama huu wa msimu wa sherehe, visa mbalimbali vya utovu wa usalama hutokea. Uhalifu huongezeka wakati kama huu wa mwaka. Je, umeweka mikakati tosha kuhakikisha kuwa uko salama katika msimu huu wa sherehe? Siku Kuu huwa ni wakati mzuri wa kupumzika na kufurahia pamoja na familia na marafiki na kushiriki chakula kizuri,” asema Bw Sahni na kutoa vidokezo kuhusu njia za kudumisha usalama msimu huu.

Hakikisha nyumbani kwako ni salama

Wakati huu wa Krismasi ni muhimu kuhakikisha kuwa nyumba yako na vitu vilivyomo ni salama.

Hakikisha milango na madirisha ya nyumba yamefungwa nyakati zote ili wezi wasiingie na kuiba. Ikiwezekana, weka ving’ora, kamera za usalama (CCTV) na taa za usalama. Vilevile, uwe mwangalifu kuhusiana na jumbe unazoweka katika mitandao ya kijamii. Kwa mfano, ukisema kuwa uko mahala ambapo ni mbali na nyumba yako, wakora wanaweza kuvamia nyumba yake na kuiba mali.

Hafla

Kuna uwezekano mkubwa kwamba huenda ukaalikwa kwa hafla ya mikutano mingi msimu huu wa sherehe kuliko wakati mwingine katika mwaka.

Jihadhari usije ukaacha vinywaji vyako katika hafla hizo bila mtu wa kukuangalia

Hakikisha hunywi pombe kupita kiasi ili usije ukajipata hatarini. Na uelekea nyumbani baada ya kuhudhuria sherehe mbalimbali. Usitembee pekee yako na hakikisha unatembea mahala penye mwangaza. Pia, usibebe chochote chenye thamani kubwa kama vile pesa nyingi au mikufu yenye thamani kubwa kwa sababu unaweza kushambuliwa na wakora.

Kuendesha gari

Siku chache kuelekea msimu wa Siku Kuu ya kukamilisha mwaka, watu wengi hufanya kazi kwa saa nyingi wakijiandaa kwa sherehe. Kwa hivyo, usiendeshe gari ukijihisi mchovu.

Ni heri usimame mahali fulani salama, ulale kidogo kabla kuendelea na safari.

Ukiendelea kuendesha gari katika hali hiyo ya uchovu ni hatari kwani unaweza kupatwa na ajali. Kulingana na takwimu kutoka idara ya trafiki asilimia 90 ya ajali hutokana na makosa ya mwanadamu.

Usiendeshe gari kwa kasi kupita kiasi katika msimu huu wa sherehe. Ni heri uwasili mahala fulani kuchelewa badala ya kuhatarisha maisha kwa kuendesha gari kwa kasi kupita kiasi.

Vile vile, ikiwezekana usiendeshe gari nyakati za usiku kwani ni rahisi kukwepa mashimo na mifugo barabarani mchana.

Mwishowe na muhimu zaidi, usiendeshe gari ukiwa mlevi au baada ya kutumia dawa za kulevya.

Ukihisi mlevi kupindukia, tafuta huduma za teksi ikusafirishe.

Watoto kutekwa nyara

Visa vya watoto kupotea katika maduka makubwa na maeneo mengine ya starehe huwa ni vingi wakati huu wa msimu wa sherehe. Watoto hupotea baada ya kutengana na wazazi wao katika maeneo kama hayo kwa sababu huwa yamejaa watu na vitu vingi vya kuzubaisha. Kwa hivyo, ewe mzazi unayependa kuandamana na watoto wako katika maeneo kama hayo hakikisha wale wadogo wako karibu nawe.

Kwa wale wakubwa, hakikisha kuwa umepanga mahali ambapo mtakutana endapo mtatengana.

Ewe mzazi, hakikisha kuwa watoto wako wanajua jina lako kamili na nambari yako ya simu. Hii itawasaidia wasimamizi wa maeneo ya sherehe kukuunganisha na mtoto wako kwa urahisi endapo atapotea.

Wafunze watoto wako kuhusu hatari ya kutembea na watu wasiowafahamu hasa katika maduka makubwa ili wasitekwe nyara kwa urahisi.

Endapo utampoteza mtoto wako, wasiliana na wasimamizi wa kamera za CCTV kubaini ikiwa wametekwa nyara au la.

Habari zinazohusiana na hii

Krismasi ya msoto