Nitafungulia Mulembe mlango wa urais – Mudavadi
Na DERICK LUVEGA
KIONGOZI wa Amani National Congress (ANC) Bw Musalia Mudavadi amezungumzia hadharani kwa mara ya kwanza yaliyojiri alipohudumu kama Makamu wa Rais mnamo 2002.
Bw Mudavadi amedai kuwa uteuzi wake uliisaidia sana jamii ya Abaluhya kupata nyadhifa kuu serikalini baada ya Kanu kushindwa na muungano wa Narc kwenye uchaguzi mkuu wa 2002.
Alisema kuwa baada yake, viongozi wengine kutoka jamii hiyo waliteuliwa kuhudumu katika nafasi iyo hiyo.
Baada ya Bw Mudavadi, marehemu Kijana Wamalwa na Bw Moody Awori waliteuliwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki kama makamu wa rais.
“Ni vizuri kuwa wa kwanza katika jambo lolote. Ndimi niliwafungulia milango nilipoteuliwa kama makamu wa rais. Vivyo hivyo, nataka kuwafungulia njia tena nitakapotwaa urais,” akasema.
Kwa hayo, Bw Mudavadi aliiomba jamii hiyo kumuunga mkono anapolenga kuwania urais mnamo 2022.
Alikuwa akihutubu katika hafla moja Jumamosi katika Kaunti ya Vihiga. Alisema kuwa hilo litaiwezesha jamii hiyo kupata nyadhifa nyingi zaidi ikiwa ataibuka mshindi.
Bw Mudavadi aliteuliwa katika nafasi hiyo na Rais Mstaafu Daniel Moi miezi kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.
Bw Mudavadi alipoteza kiti chake cha ubunge katika eneo la Sabatia kwa kuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta aliyewania urais kwa tiketi ya Kanu.
Bw Mudavadi pia alihudumu kama Naibu Waziri Mkuu kati ya 2007 na 2013 kwenye Serikali ya Muungano kati ya Bw Kibaki na kinara wa ODM Raila Odinga.