• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 AM
2019: Jumla ya wazee 46 waliuawa wakidaiwa kuwa wachawi

2019: Jumla ya wazee 46 waliuawa wakidaiwa kuwa wachawi

Na MAUREEN ONGALA

JUMLA ya wazee 46 waliuliwa katika Kaunti ya Kilifi mwaka huu kwa madai potovu kwamba walikuwa wachawi, kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI).

Ijapokuwa idadi hiyo imepungua kutoka wazee 99 mwaka wa 2017 na wazee 79 mwaka wa 2018, suala hilo bado ni la kutisha kwani idadi ya mwaka huu ni sawa na kuuawa kwa wazee wanne kila mwezi au mmoja kila wiki kwa mwaka mzima.

Afisa wa Upelelezi wa Jinai katika Kaunti ya Kilifi (CCIO), Bw Edwin Kamau, alisema idadi ya mauaji imekuwa ikipungua kwa sababu ya hamasisho linalofanywa na walinda usalama pamoja na wadau wengine katika jamii kuhusu hitaji la kutumia sheria kutatua mizozo ya umiliki wa ardhi badala ya kusingizia kwamba wazee ni wachawi ilhali lengo ni kunyakua ardhi zao wanapouawa.

“Mtu yeyote mkongwe huwa anahusishwa na uchawi Kilifi kisha baadaye anauawa. Tunahamasisha jamii kupitia kwa mabaraza kwamba wajiepushe na tamaduni zilizopitwa na wakati,” akasema afisini mwake.

Wazee wa Kaya mnamo Jumamosi walitaka wazee waruhusiwe kutatua kesi za mizozo ya ardhi ambayo husababisha mauaji kwa madai ya uchawi.

Mratibu wa baraza la wazee wa Kimijikenda, Tsuma Nzai alisema tayari makabila matano ya jamii ya Mijikenda yameathiriwa na mauaji hayo.

“Mauaji haya yalianza na Wagiriama, kisha Wachonyi na hata Warabai wakaanza kuathiriwa. Sasa yameenea hadi kwa Waduruma na tuna wasiwasi na itabidi hatua kali zichukuliwe ili kukomesha tabia hiyo,” Bw Nzai alisema.

Alisema wazee wamejitolea kujaribu kushughulikia kesi ndogo za uhalifu lakini hawaruhusiwi kushughulikia masuala ya ardhi ambayo yanahusiana na uchawi.

“Serikali hairuhusu wazee kushughulikia kikamilifu masuala ya ardhi na uchawi na hii inakuwa tishio la usalama katika jimbo. Ipo haja ya wao kujulisha wanajamii kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa baraza la wazee na pia wapewe uwezo wa kutatua migogoro,” alisema.

Aliongeza kuwa kila Jumanne wazee wa Kimijikenda huendesha korti zao katika misitu ya Kaya.

“Wanashughulika tu na kesi za ndoa kama mwanamume kupatikana na mke wa mtu mwingine na au wazazi ambao wanalazimisha wasichana wachanga kuolewa mapema kwani ni kinyume cha sheria. Kesi hizi hushughulikiwa tu hadi kiwango cha mzee wa kijiji. Kesi yoyote ambayo inamhusisha chifu huchukuliwa kuwa ya jinai na hupelekwa katika kituo cha polisi ili wachukue hatua,” alisema.

Kwa mujibu wa Nzai, mambo yanayohusu ardhi pia yanapaswa kushughulikiwa na mabaraza ya wazee.

“Watu wanapaswa kuelewa historia ya ardhi yao na pale ambapo mipaka iko. Suala ambapo wanasorveya wanakuja kupima ardhi inaleta migogoro mingi,” alisema.

Hapo zamani, iwapo kungekuwa na mzozo wa ardhi, wazee kutoka pande zote mbili wangekuja pamoja na kujadili suala hilo. Baada ya kusuluhisha tofauti husika wangechinja mbuzi walioletwa na wahusika wangeruhusiwa kuenda makwao kwa amani.

Bw Nzai alisema wameshughulikia kesi zaidi ya 400 za madai ya uchawi tangu 2013 hadi sasa. Baadhi ya wazee wamepelekwa katika kituo cha uokoaji cha Kaya Godoma katika eneo la Mrima wa Ndege huko Ganze huku akiongeza kuwa ipo miaka ambapo wazee wengi huuliwa kuliko mingine.

You can share this post!

Nitafungulia Mulembe mlango wa urais – Mudavadi

2019: Vita dhidi ya mihadarati Pwani vilififia

adminleo