• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
2019: Vita dhidi ya mihadarati Pwani vilififia

2019: Vita dhidi ya mihadarati Pwani vilififia

NA MOHAMED AHMED

AGOSTI 13 itasalia kwenye kumbukumbu za Wakenya, hasa Wapwani mwaka huu unapoelekea kukamilika.

Mwendo wa saa nane tarehe hiyo polisi zaidi ya 30 walizingira nyumba ya bwenyenye Ali Punjani kwa madai ya kuhusika kwake na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Polisi walifika hapo saa chache baada ya Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiang’i kufika katika ukanda wa Pwani na kutangaza vita vipya dhidi ya mihadarati.

Operesheni ya polisi kufika kwenye jumba hilo la kifahari ilileta hisia ya mwamko mpya katika vita dhidi ya mihadarati.

Kufika kwa polisi kwenye makao hayo eneo la Nyali kulijiri siku moja tu baada ya OCS wa kituo cha polisi cha Kizingitini Shadrack Mumo kukamatwa kuhusiana na kesi inayohusiana na biashara ya dawa za kulevya.

Ni wakati wa kamata kamata hiyo ambapo diwani wa Bofu Ahmed Salama naye alikamatwa kwa madai ya kuhusika kwake katika biashara hiyo.

Vile vile mamia ya wauzaji wa dawa za kulevya walikamatwa huku maafisa wa usalama wakinasa bangi, heroini na kokeni ya kutosha.

Miongoni mwa wengine walioshikwa wakati huo ni pamoja na afisa wa polisi wa kike aliyedaiwa kuhusika katika biashara hiyo haramu.

Ni kamata kamata hiyo ambayo ilionyesha kuwa vita hivyo vimepata nguvu mpya. Hata hivyo kufikia sasa tunapoelekea mwaka mpya, serikali haiwezi kujipiga kifua kuwa imepambana na vita hivyo vya kutosha.

Akizungumza jijini Nairobi mwezi mmoja baadaye Bw Matiang’i aliweka wazi kuwa kuna watu zaidi ya 30 ambao wana nguvu za kibiashara na zile za kisiasa na wanachunguzwa kwa kuhusika kwao kwenye biashara hiyo.

“Hao watu si Wakenya wa kawaida ni watu wenye hadhi, lakini kwenye vita hivi hatutochagua. Saa hii bado uchunguzi unaendelea na wakati mwafaka ukifika basi tutatekeleza hatua zifaazo,” akasema Bw Matiang’i.

Huku vita hivyo vilivyokuwa vimelenga kanda ya Pwani vikiwa vinaendelea, walanguzi wa dawa nao walisemekana kuweka onyo kwa serikali.

Hii ni baada ya afisa wa polisi Hesbon Okemwa aliuawa mnamo Oktoba eneo la Lamu.

Mwili wake ulipatikana siku chache baada ya afisa huyo ambaye alitajwa kuwa msitari wa mbele katika vita dhidi ya mihadarati eneo hili kuripotiwa kupotea.

Kifo chake kilijiri miezi kadhaa baada ya afisa wa kuhusika na kazi za jamii naye pia kuawa huku ikiaminika kuwa ni kwa sababu ya misimamo yake dhidi ya biashara hiyo eneo la Lamu.

Hali hii imebainisha kuwa vita hivyo si rahisi kwa maafisa wa usalama ambao wamejitolea kupambana na suala hilo sugu.

Hii ni hata masuali yakiibuka iwapo serikali ipo na nia ya ukweli katika kumaliza donga hilo katika kanda ya Pwani.

Wakati Wakenya hususan Wapwani wanapoelekea mwaka mpya ni matumaini ya wengi kuwa vita hivyo ambavyo vimeonekana kufifia katika siku za hivi majuzi vitaendelezwa kwa dhati.

Macho bado yameelekezwa kwa wasimamizi wa usalama eneo hili wakiongozwa na kamishna wa kanda ya Pwani John Elung’ata na mwenzake kamanda wa polisi Rashid Yakub.

You can share this post!

2019: Jumla ya wazee 46 waliuawa wakidaiwa kuwa wachawi

2019: Wabunge 13 ambao wamekuwa mabubu bungeni tangu...

adminleo