• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
2019: Wabunge 13 ambao wamekuwa mabubu bungeni tangu waapishwe

2019: Wabunge 13 ambao wamekuwa mabubu bungeni tangu waapishwe

Na CHARLES WASONGA

MDAHALO mkali uliibuka mwaka huu kuhusu suala zima la utathmini wa utendakazi wa wabunge na maseneta baada ya kubaini kuwa ni wachache tu ambao hushiriki mijadala bungeni huku wengi wao “wakizembea kazini”.

Hii ni baada ya shirika la Mzalendo Trust ambalo hufuatilia utendakazi wa wabunge kutoa ripoti iliyofichua kwamba kufikia Juni 30, 2019 takriban wabunge 13 hawakuwa wamechangia hoja au miswada yoyote tangu 2017 walipoapishwa kuanza kuhudumu.

Miongoni mwa wabunge hao, kulingana na ripoti hiyo, walikuwa Oscar Sudi (Kapseret), Samuel Arama (Nakuru Mjini Magharibi), Aduma Owuor (Nyakach), Justus Kizito (Shinyalu), Alfred Sambu (Wabuye Magharibi), Alex Kosgey (Emgwen), James Wamacukuru (Kabete) na Charles Kamuren (Baringo Kusini).

Nao Wabunge Wawakilishi wa Kaunti ambao ilibaini hawajatamka lolote katika ukumbi wa mijadala tangu waapishwe rasmi ni pamoja na Anab Mohamed (Garissa), Lilian Tomitom (Pokot Magharibi), Irene Kasalu (Kitui), Jane Wanjiku (Embu) na Jane Chebaibai (Elgeyo Marakwet).

Na katika Seneti, Seneta wa Baringo Gideon Moi na mwenzake wa Meru Mithika Linturi ni miongoni mwa wale ambao michango yao kwa mijadala na hoja ni finyu zaidi ikilinganishwa na wenzao.

Wengine ni; Issa Juma Boy (Kwale), Anwar Loitiptip (Lamu), Philip Mpaayei (Kajiado), Abdullahi Ibrahim (Wajir) na maseneta wateule Millicent Omanga, Christine Gona, Mercy Chebeni, Victor Prengei na Falhada Dekow.

“Kinaya ni kwamba baadhi ya wabunge na maseneta wanyamavu ukumbini ni wanenaji hodari katika makwaa mbali mbali nje ya bunge. Miongoni mwao ni Mbw Sudi, Arama, Kizito, Linturi, Moi na Bi Omanga,” Mkurugenzi Mkuu wa Mzalendo Trust Caroline Gaita alisema.

Kujitetea

Lakini Bw Sudi, ambaye pia hushirikia mijadala kuhusu masuala mengi ya kitaifa kupitia mitandao ya kijamii alipuuzilia mbali ripoti hiyo akisema “nilichaguliwa kuhudumia watu wa Kapseret wala si kuzungumza bungeni.”

Wabunge wengine waliokosoa tathmini hiyo walisema michango yao katika vikao vya kamati mbalimbali za mabunge hayo mawili.

“Ripoti kama hii ambayo inaangazia michango yetu ukumbini pekee haina maana na inapasa kupuziliwa kabisa. Asilimia 80 ya kazi ya wabunge huendesha katika vikao vya kamati wala sio ukumbini,” akasema Bw Kosgey ambaye ni mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Mazingira.

You can share this post!

2019: Vita dhidi ya mihadarati Pwani vilififia

Maandalizi ya Krismasi yashika kasi

adminleo