Mbunge awapa wakazi Krismasi,awarai viongozi wengine kufanya hivyo

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuwajali wale wasiojiweza hasa wakati huu wa sikuu ya Krismasi kulingana na mbunge wa Ruiru, Bw Simon King’ara.

Amesema kuna watu wengi maeneo ya mashinani eneo la Ruiru, ambao wangetaka kupewa misaada lakini hakuna watu wanaowajali kwa vyovyote vile.

Mwishoni mwa wiki mbunge huyo alizuru vijiji kadha kwa lengo la kutoa vyakula vya sikukuu ya Krismasi.

Wakati wa ziara hiyo aliweza kuwafikia mayatima, wakongwe, wagonjwa, walemavu na watoto ili kuwafadhili na vyakula vya sikukuu.

Bw King’ara aliwakabidhi unga wa chapati, mafuta ya kupikia, sabuni, sukari na mchele.

“Ninatoa mwito kwa viongozi wengine na wahisani popote walipo wafanya jambo kwa kuwakumbuka wote wasiojiweza kimaisha hasa wakati huu wa sikukuu. Kile kidogo mtu anacho anastahili kuisambaza pia kwa wengine,” alisema Bw King’ara.

Alitoa mwito kwa wakazi wa Ruiru washerehekee sikukuu kwa amani na wajiepushe na maovu yanayoweza kuwafikia.

“Wakati kama huu kila mmjoja anastahili kujiunga na familia yake ili kusherehekea sikukuu ya krisimasi kwa amani,” alisema mbunge huyo na kuongeza “lakini tusimsahau mwenyezi Mungu ambaye ameweza kutufikisha mahali hapa tukamaliza mwaka mzima bila matatizo mengi.”

Bi Mary Wangari wa miaka 68 alimpongeza mbunge huyo kwa kuonyesha ukarimu kwa watu wake na hiyo ni upendo mzuri unaostahili kupongezwa.

“Sisi kama wakazi wa Ruiru tunampongeza mbunge wetu kwa ukarimu aliyotuonyesha wa kutuletea sikukuu. Hatutasahau kumuombea ili aweze kutuongoza kwa unyenyekevu na upendo,” alisema Bi Wangari.

Habari zinazohusiana na hii

Krismasi ya dhiki

Krismasi ya msoto