• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Madiwani 18 wala njama ya kumwokoa Sonko

Madiwani 18 wala njama ya kumwokoa Sonko

Na COLLINS OMULO

MADIWANI 18 wamekula njama ya kutibua jaribio la kumtimua Gavana wa Nairobi Mike Sonko, imefichuka.

Madiwani hao sasa wanapanga kusafiri nje ya nchi kwa lengo la kuhakikisha kuwa hoja ya kumtimua Sonko inagonga mwamba.

Tayari madiwani wa ODM wamempa makataa ya siku saba Spika wa Bunge la Kaunti, Bi Beatrice Elachi kuhakikisha kuwa anaandaa kikao cha dharura kujadili masaibu yanayokumba Kaunti ya Nairobi.

Baadhi ya madiwani wanapanga kuwasilisha mswada wa kumtimua Gavana Sonko baada ya korti kumzuia kwenda afisini mwake mnamo Desemba 6 hadi pale kesi ya ufisadi inayomkabili itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Endapo madiwani hao 18 watasafiri nje ya nchi, basi huenda idadi ya wanaounga hoja ya kumtimua Gavana Sonko ikakosa kufikia theluthi mbili.

Kaunti ya Nairobi ina madiwani 123 na wanahitajika 82 kupitisha hoja ya kumtimua Bw Sonko.

Katika Barua iliyoonwa na Taifa Leo, madiwani hao 18 wanatarajiwa kuelekea Dubai, Milki za Kiarabuni (UAE) wakiandama na wafanyakazi watatu wa Bunge la Kaunti.

Ziara hiyo tayari imeidhinishwa na katibu wa wizara ya Fedha ya Kaunti ya Nairobi.

Barua hiyo imetokea katika afisi ya karani wa bunge la kaunti na imeandikiwa Katibu wa Kaunti ya Nairobi.

Barua hiyo inataka serikali ya Kaunti ya Nairobi kuwasaidia madiwani hao ambao wamealikwa na taasisi mbambali nchini Dubai, kusafiri. Madiwani hao wanafaa kuwa nchini Dubai kati ya Desemba 19 na 29, mwaka huu.

Serikali ya Kaunti ilifaa kuwalipia nauli ya ndege na hoteli ambayo wataishi.

Wanaotarajiwa kusafiri ni Jared Okode (Mathare Kaskazini), Maurice Gari (Nairobi Magharibi), Osman Khalif (South C), Francis Otieno (Dandora Area IV), Nicholas Okumu (Lower Savannah), diwani wa Imara Daima, Bw Kennedy Obuya, Kennedy Oyugi (Nyayo Highrise) na David Okelo (Huruma) wote wa chama cha ODM.

Upande wa Jubilee ni Kiongozi wa Wengi Charles Thuo, Paul Ndung’u (Pumwani), Patriciah Mutheu (Mlango Kubwa), Joseph Wambugu (Karura), Kabiru Muchene (Uthiru Ruthimitu), Mark Ndugu (Maringo Hamza), Julius Njoka (Kariobangi Kaskazini), Madiwani Maalumu Joyce Kamau na Millicent Jagero.

Wafanyakazi wa Bunge la Kaunti wanaotarajiwa kusafiri na madiwani hao ni Kaimu Karani wa Bunge la Kaunti Monicah Muthami, Asman John na Joseph Katoloki.

You can share this post!

Mshukiwa wa sakata ya Kimwarer na Arror abambwa JKIA

Kalonzo aomba msamaha kuungana na Uhuru

adminleo