Mutua sasa atishia kumwaga mtama kuhusu ghasia za 2007
Na WANDERI KAMAU
GAVANA Alfred Mutua wa Machakos amedai kuna mengi anayofahamu kuhusu matukio ya ghasia za baada ya uchaguzi tata wa 2007/2008 ambapo zaidi ya Wakenya 1,300 waliuawa, ambayo atafichua karibuni.
Katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga Jumapili usiku, Dkt Mutua alidai alikuwa shahidi katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) na kuna mengi ambayo hayajafichuliwa kwa umma.
“Nilikuwa shahidi katika ICC. Niliandikisha taarifa ambazo zipo hadi sasa. Nilikuwa katika serikali wakati huo, hivyo ninafahamu undani kuhusu matukio hayo. Ukweli utadhihirika,” akasema.
Ghasia hizo zilitokea katika sehemu mbalimbali nchini baada ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa 2007 na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya (ECK) Bw Samuel Kivuitu.
Kinara wa ODM Raila Odinga alidai kwamba Bw Kibaki alishirikiana kisiri na tume hiyo kumwibia kura kwenye uchaguzi huo, alioshikilia ndiye aliibuka mshindi.
Utata uliotokea uliwafanya Wakenya sita kufunguliwa mashtaka katika ICC, kwa tuhuma za kuchochea na kufadhili ghasia hizo.
Sita hao walijumuisha Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto, aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Bw Francis Muthaura, aliyekuwa Kamishna wa Polisi Hussein Ali, waziri wa zamani Bw Henry Kosgey na mwanahabari Joshua arap Sang.’
Na ingawa mashtaka yao yalifutiliwa mbali baada ya ushahidi uliotolewa kukosa kuthibitisha ushiriki wao, baadhi ya wadadisi wanasema kuwa itachukua muda mrefu kovu lililoachwa na ghasia hizo kuondoka, hasa miongoni mwa wale walioshuhudia.
Dkt Mutua, aliyehudumu kama Msemaji Mkuu wa Serikali, alieleza vile baadhi ya Wakenya walijaribu kumfikia kumwomba usaidizi.
“Nakumbuka nikipokea simu za Wakenya kutoka eneo la Bonde la Ufa wakisema kuwa wamevamiwa kwa kuwa wa jamii tofauti. Ni matukio yanayonisumbua hadi sasa,” akaeleza.
Alisema kuwa lazima waliohusika walipie makosa waliofanya, licha ya miito ya maridhiano miongoni mwa Wakenya.
“Lazima wale waliopanga na kufadhili ghasia hizo wawajibike. Ingawa kuna miito ya maridhiano kwa Wakenya, lazima kila mmoja aliyehusika awajibike,” akasema.