• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
SYOKAU NZOMO: Namshukuru Mola nang’aa kwa usanii wa injili licha ya dhuluma nyumbani

SYOKAU NZOMO: Namshukuru Mola nang’aa kwa usanii wa injili licha ya dhuluma nyumbani

Na JOHN KIMWERE

NI ndoto ya kila msanii kuona anabobea katika kazi zake na kutambulika kote duniani. Aidha, kila mwimbaji anayeibukia huwa na maazimio ya kughani tambo zenye maudhui ya kuchota nyoyo za wengi huku akidhamiria kutinga upeo wa mastaa waliotangulia.

Justina Syokau Nzomo ni miongoni mwao wasanii wanaokuja ambao hutunga muziki wa kumtukuza Mungu. Ndani ya miaka kumi sasa amekuwa katika harakati za kuhubiri injili ya Mungu kupitia tambo za utunzi wake.

Anadokeza kuwa baadhi ya nyimbo zake zimeibuka muhimu kwa kuwajenga kiroho kondoo wa Mungu. Hayo tisa. Kumi anasema mwaka huu (2019) umekuwa wa ushindi kwake.

”Nashukuru Mungu maana katika muziki najivunia kushinda tuzo mbili mwaka huu,”anasema na kuongeza kuwa ufanisi huo ulianza kuonekana miaka mitano iliyopita.

Nyimbo yake iitwayo ‘Mama’ ilishinda tuzo kwenye kipengele cha ‘Eastern Song of the Year’ katika tuzo za Kenya Gospel Music Awards (KEGMA) zilizoandaliwa jijini Nairobi.

Mapema mwezi huu alishinda tuzo nyingine kwenye kipengele cha ‘Best Gospel Artist of the Year Kenya’ katika tuzo za Mziki Africa Awards zilizofanyika mjini Mombasa.

Anasema meneja wake, Fred Oketch amechangia kwa kiwango fulani ufanisi wake katika muziki.

”Nimekuwa naye kwa miezi minane ambapo bila kumpigia chini amenisaidia zaidi kwa mawaidha, kunielekeza la kufanya pia sapoti hapa na pale. Bila shaka siwezi kuweka katika kaburi la sahau jamii yake imekuwapo tayari nyakati zote nikihitaji msaada,” akasema.

Kisura huyu amefaulu kughani na kurekodi takribani fataki 76 (audio na video) zinazopatikana kupitia mtandao wa YouTube.

Kufanya vizuri

Kwa jumla nyimbo nne zake zimepokelewa vizuri na wafuasi wa muziki wa Mungu vile vyombo vya habari hpa nchini. Tambo hizi zikiwa ‘Nataka Niishi,’ na ‘Ng’ang’ana’ alizoachia mwaka 2014 na 2017 mtawalia.

Bila kupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa tugho mbili za mwaka huu ‘Mama,’ na ‘Kilisimasi’ zinaendelea kufanya vizuri.

Akipiga soga na mwandishi wetu, msanii huyu alisema, ”Wimbo wa Mama unazidi kupangawisha wapenzi wa burudani ya muziki wa injili maana unawatia wanawake moyo pia kuwatambua kuwa viumbe vya dhamani kubwa kuliko shaba katika familia.”

Pia nyimbo hiyo imechangia mwimbaji huyu kupata shoo nyimbo katika maeneo tofauti kote nchini kando na kumfikisha kiwango cha kuanza kuibuka maarufu miongoni mwa wenzake waliotangulia.

Mume mkorofi

”Nimewahi kuwa katika ndoa ndani ya mwaka mmoja ila kiukweli nilipitia mapigo makali lakini Mungu ni mwema alinipigania kwa udi na uvumba na kunisaidia kujinasua dhidi ya minyororo ya muovu shetani,” anasema dada huyu mzawa wa Mua Hills, Kitanga, Machakos.

Anadai mumewe alikuwa balaa nyakati zote hali iliyochangia kuvunjika kwa ndoa yao. Anahimiza wenzake watafakari kwanza kabla waingie katika maisha ya ndoa, ili kujiepusha dhidi ya matendo ya aibu kwa wanandoa na kondoo wa Mungu.

Syokau anashusha shukran za dhati kwa wafuasi wake wote kwa kumpa sapoti ili kuendeleza shughuli za muziki tangia alipoachika.

Kadhalika anashukuru mchungaji wake, Chris Musau wa kanisa la Redeemed Gospel, bila kusahau mwezake mtumishi wa Mungu, Lucy Natasha kwa sala zao pia kumtia motisha kuwa atainuka katika muziki.

Binti huyu kamwe sio mchoyo wa mawaidha. Anawataka wasanii wanaokuja wafahamu jukwaa la muziki limejaa pandashuka tele lakini wasivunjike moyo mbali wavumilie na kumtumaini Mungu aliye muweza wa yote.

Aidha anawasihi wawe wakitunga nyimbo zilizo na mafundisho ya kimaadili katika za kuibadili jamii kwa jumla.

Fakati zake ‘Nataka Niishi’ ‘Hamu’  zilipata nafasi nzuri na kuchezwa kwenye runinga mbali mbali ikiwamo K24, KBC, NTV Password, QTV Chee, Njata TV, Sayari, ATG TV, GBS TV, UTV, Hope TV, Citizen TV na Kingdom TV.
Kati ya nyimbo zingine za utunzi wake ni kama  ‘Hamu’ ‘Ndukandie,’ ‘Future Nzuri,’ ‘Mbele’, ‘Nimeinuliwa,’ ‘Mwache Yesu,’ ‘Neno’ na pia ‘Unachopanda.’
Dada huyu pia anasema anapenda kujifunza kutoka kwa wenzake ambapo anavutiwa na kazi ‘Bwana Yesu,’ ‘Najua mkombozi wangu,’ na zile za ‘Sitarudi kuwa vile,’ na ‘Mambo yabadilika’, za wanamuziki wa hapa Kenya Eunice Njeri na Hellena Ken mtawalia.
Aidha anapangawishwa na fataki za waimbaji wa Bongo, Bahati Bukuku kama ‘Esther,’ ‘Ukiinuliwa na mwanadamu’ pia anaguswa zaidi na muziki wa ‘Wololo’ na ‘Nibebe’ kazi yake mwimbaji maarufu Rose Muhando.
Kuhusu changamoto anasema kwa sasa anaendelea vizuri tatizo kubwa ni uchumi unavyoendelea kupiga wananchi.

You can share this post!

Maendeleo yalivyokwama Zimmerman kutokana na mzozo wa ardhi

AKILIMALI: Kilimo cha matunda kinavyowafaa wakulima...

adminleo