• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
Shamrashamra za Krismasi zanoga jijini Bethlehemu

Shamrashamra za Krismasi zanoga jijini Bethlehemu

Na AFP

TANGU Jumatatu, mji wa Bethlehemu ambao unatambuliwa na Wakristo kama mahala ambapo Yesu alizaliwa umekuwa ukijiandaa kuwapokea mahujaji kutoka kote ulimwenguni kuja kusherehekea Krismasi katika mji huo mtakatifu.

Mji huo ulioko katika eneo la West Bank linalodhibitiwa na Israeli umekuwa ikiandaa sherehe mbali mbali ndani ya nje ya Kanisa lijulikanalo kama Church of Nativity, ambalo lilijengwa mahala panapoaminika kuwa Yesu alizaliwa.

Mnamo Jumatatu alasiri, mamia ya watalii na wenyeji walikongamana nje ya Kanisa hilo ambapo mti wa Krismasi wenye urefu wa mita 15 (futi 50).

Watoto waliovalia kama Baba Krismasi (Santa Claus) walikuwa wakicheza pembeni huku wafanyakazi wakiunganisha vipaza sauti na televisheni kubwa. Wimbo wa Krismasi ulikuwa ukichezwa katika uwanja huo.

Askofu Mkuu Pierbattista Pizaaballa, kiongozi wa kanisa jijini Jerusalem na afisa mwenye cheo cha juu zaidi katika Kanisa Katoliki katika Mashariki, alikuwa akitarajiwa kusafiri kutoka Yerusalem hadi Bethlehem jana asubuhi.

Alikuwa amepengiwa kuongoza ibada ya usiku katika Church of the Nativity, ambayo Waziri Mkuu wa Palestine Mahmud Abbas anatarajiwa kuhudhuria.

Kanisa la kwanza lilijengwa mahala hapo katika karne ya nne (4), japo lilijengwa upya baada ya mkasa wa moto uliotokea katika karne ya sita (6).

Mji wa Bethlehem ni karibu na Jerusalem, lakini miji hiyo imetenganishwa na ua uliojengwa na Israeli.

Idadi ndogo ya Wakristo kutoka Ukanda wa Gaza watahudhuria sherehe hiyo ikilinganishwa na miaka ya nyumba.

Hii ni kwa sababu Israeli imetoa idhini kwa watu 200 pekee miongoni mwa 900 waliotuma ombi, akasema Waldie Abunassar, mshauri wa viongozi wa Kanisa katika mji wa Bethlehem.

Maeneo ya Palestina ya West Bank na Gaza yanametenganishwa na eneo linalokaliwa na Israeli na ili mtu avuke kati ya maeneo hayo anahitaji kibali, ambacho huwa ni ngumu kupata.

Abunassar alisema Krismasi inasalia kuwa wakati wa matumaini.

“Mji mtakatifu sio tu mahala pa kuzaliwa na kusulubishwa kwa Yesu, vile vile ni mahala pa kufufuka kwake,” akaambia shirika la habari la AFP.

“Licha ya changamoto, magumu, machungu na shida tunazokumbana nazo, tumeweka matumaini yetu kwa Mungu na watu wetu,” Abunassar akaongeza.

Kwengineko, katika mji wa Gaza nchini Palestina, Hanadi Missak na familia yake jana walikuwa wamejiandaa kwa Krismasi. Hii ni licha ya kwamba hana furaha kwamba atasherehekea siku kuu hiyo nyumbani kwake bila kusafiri hadi Bethlehem.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 48 ni miongoni mwa mamia ya Wakristo kutoka Ukanda wa Gaza ambao waliwasilisha ombi la kusafiri hadi eneo la West Bank kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu lakini wakanyimwa idhini na Israeli.

Viongozi wa Kanisa pia walilalamikia ugumu wa kupata idhini ya usafiri, tofauti na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Nilikuwa nikitarajia kusafiri hadi Bethlehemu, lakini sijafanikiwa,” Missak ambaye ni naibu wa mwalimu mkuu katika shule moja ya Kikristo katika eneo la Gaza, akaambia AFP.

Zaidi ya Wakristo 1,000 wanaishi katika eneo la Gaza ambako kuna jumla ya watu milioni mbili waliosongamana katika eneo hilo lenye urefu wa kilomita 40 na upana wa kilomita chache tu.

Eneo la Gaza linaongozwa na kundi la Kiislamu la Hamas. Ambalo Israeli inasuta wanachama wake kwa kutumia vibaya mpango huo wa utoaji leseni kupanga mashambulio dhidi ya raia wake (Israeli).

Hadi jana jiono Bw Abubassar bado alikuwa na wingi wa matumaini kwamba Wakristo zaidi watapewa leseni za kwenda Bethlehem.

“Tulipewa ahadi hiyo na asasi mbalimbali za Israeli…. Lakini Krismasi inaanza kesho (leo),” akasema jana akiongeza kuwa, “tunashikilia kuwa hii ni haki yetu ya kimsingi na inapasa kuheshimiwa.”

Israel inashikilia kuwa inahitaji kudhibiti wa ukanda wa Gaza ili kuwatenda wanamgambo wa Hamas.

Zamani, utawala wa Gaza umekuwa ukifanya sherehe kubwa za Krismasi, lakini sherehe hizo zilisitishwa baada Hamas kuidhibiti mnamo 2007.

You can share this post!

AKILIMALI: Arejea nchini kutoka China kufunza vijana jinsi...

Atisha kukausha asali Krismasi

adminleo