• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Rigathi Gachagua amwomboleza mamaye

Rigathi Gachagua amwomboleza mamaye

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Mathira Rigathi Gachagua anaombolewa mamake, Martha Kirigo Gachagua aliyefariki Jumatatu, Desemba 23, 2019.

Katika ujumbe katika ukurasa wake wa Facebook, mbunge huyo wa chama cha Jubilee alimtaja kama mama mwenye bidii aliyewalea na ndugu zake hadi wakawa “viongozi wa kutajika”.

“Mama yetu, Martha Kirigo Gachagua aliendea kuwa na Bwana jana usiku. Japo, tumepatwa na huzuni, tunasherehekea maisha bora yenye maadili tuliyoishi naye,” akasema.

“Miaka 89 aliyoishi dunia ilikuwa yenye baraka kubwa kwetu kama watoto wake na familia nzima. Roho ya Mama yetu ipumzike penye amani daima,” Bw Gachagua akaomboleza.

Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga pia alimwomboleza mamake Rigathi akimsifu kama nguzo muhimu katika jamii.

“Naungana na familia ya Rigathi Gachagua, na familia nzima ya Gachagua, jama, marafiki na watu wa Mathira kuomboleza mama yao mpendwa, Martha Kirigo Gachagua ambaye amefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.

“Martha amekuwa nguzo kuu katika familia hii ambayo iliipa Nyeri gavana wake wa kwanza, marehemu Nderitu Gachagua. Vile vile, familia hii iliipa eneo bunge la Mathira wabunge wawili,” akasema Bw Kahiga, akiahidi kwamba serikali yake itasaidia familia hiyo katika matayarisho ya mazishi.

Marehemu gavana Gachagua alifariki mnamo February 2017 katika hospitali moja jijini London Uingereza, alikolazwa akiugua maradhi ya saratani kongosho (pancreatic cancer).

Marehemu Martha Kirigo ni mkewe marehemu Nahashon Gachagua Reriani.

You can share this post!

AKILIMALI: Manufaa ya mianzi kwa maisha ya binadamu

Krismasi: Huduma za paspoti zasitishwa hadi Ijumaa

adminleo