Habari MsetoSiasa

Vigogo wa kisiasa wanavyomumunya Krismasi

December 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WANDERI KAMAU

VIONGOZI mbalimbali wa kisiasa nchini wanatarajiwa kujiunga na Wakenya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi leo.

Kinara wa ODM Raila Odinga anatarajiwa kujiunga na familia yake katika shamba lake la Opoda liliko Bondo, Kaunti ya Siaya kwa sherehe hizo.

Akizungumza na Taifa Leo jana, msemaji wake, Bw Dennis Onyango alisema kwamba Bw Odinga atatumia muda huo kuwa na familia yake.

Ijapokuwa Ikulu ilikataa kufichua mipango ya Rais Uhuru Kenyatta kwa sherehe za Krismasi, alituma ujumbe wa heri njema kwa Wakristo wote nchini, akiwatakia neema kwenye sherehe hizo.

“Tunaposherehekea Krismasi hii pamoja na Mwaka Mpya, ni maombi yangu kuwa tutatumia nguvu zetu kuiboresha Kenya kuwa makao bora kwa vizazi vijavyo,” akasema Rais.

Rais pia aliwatakiwa Wakenya Mwaka Mwema wa 2020.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka naye atakuwa jijini Nairobi, ambapo pia atakuwa na familia yake.

Kulingana na washirika wake wa karibu waliohojiwa na Taifa Leo, Bw Musyoka atachukua muda wake kupumzika kutoka kwa majukumu yake mengi kitaifa na kimataifa.

Itakuwa vivyo hivyo kwa kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Bw Musalia Mudavadi, ambapo atakuwa nyumbani kwake katika eneo la Mululu, Kaunti ya Vihiga, atakapojumuika na familia.

Baada ya sherehe hizo, Bw Mudavadi anatarajiwa kujiunga na viongozi wengine katika eneo la Magharibi kesho kwenye tamasha za jamii ya Wamaragoli, ambazo huandaliwa kila mwaka.

Katibu Mkuu wa ANC Bw Barrack Muluka alisema kuwa baadaye, Bw Mudavadi ataelekea katika eneo la Pwani kwa sherehe za Mwaka Mpya.

Haikubainika mara moja atakakokuwa Naibu Rais William Ruto, ijapokuwa huenda akawa nyumbani kwake Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu.