• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
Mauzo duni Krismasi, wafanyabiashara waumia

Mauzo duni Krismasi, wafanyabiashara waumia

CONSTANT MUNDA na SIAGO CECE

WAFANYABIASHARA walipata pigo baada ya Wakenya kupunguza matumizi ya fedha kwa sherehe za Krismasi mwaka huu, ithibati ya kudorora kwa uchumi.

Mauzo katika katika maduka makuu na wauzaji wa nguo na vyakula kama vile kuku, yalikuwa duni wakati wa sherehe za Krismasi.

Kupungua kwa mauzo wakati wa sherehe za Krismasi kunatokea wakati ambapo mashirika mbalimbali yameripoti kupungua kwa mapato huku baadhi ya wafanyakazi wakitimuliwa na waliosalia wakinyimwa nyongeza ya mishahara.

Serikali ya kitaifa na kaunti pia zimechelewesha malipo ya jumla ya Sh100 bilioni zinazodaiwa na wakandarasi. Baadhi ya wakandarasi wameshindwa kulipa mikopo ya benki hivyo mali yao kupigwa mnada na kusitisha operesheni.

Kutokana na hilo, takwimu za Benki Kuu ya Kenya (CBK) zinaonyesha kwamba fedha zinazotumiwa na Wakenya nje ya benki zimepungua hadi Sh176.9 bilioni. Hiyo ndiyo mara ya kwanza kwa fedha zinazozunguka miongoni mwa Wakenya, nje ya benki, kupungua kwa kiasi hicho tangu Julai 2015.

Sekta ya utalii haikusazwa kwani uchunguzi wa Taifa Leo ulibainisha kwamba katika maeneo ya Pwani, kulikuwa na wageni wachache hotelini ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Tofauti na miaka iliyopita ambapo hoteli zilikuwa zikijaa mapema msimu wote wa Krismasi, uchunguzi wetu ulionyesha bado kuna nafasi tele katika hoteli za Travelers, Pride in Paradise, Sarova Whitesands, Nyali Beach na Baobab.

Kusini ya Pwani, nafasi bado zipo katika hoteli ya Diani Reef, Leisure Lodge na Leopards.

“Bado tuna matumaini wageni watakuja kwa sherehe za kufungua mwaka,” mkuu wa mauzo katika hoteli ya Travelers, Bw Wafula Waswa alisema, akithibitisha wageni mwaka huu ni chini ya asilimia 67.

Maduka makuu yalisema kuwa kulikuwa idadi kubwa ya wateja lakini walinunua vitu vichache tu.

Wateja walikuwa wakinunua bidhaa za kawaida kama vile mkate, maziwa, sukari.

Dan Githua, Mkurugenzi Mkuu wa Tusker Mattresses Ltd, alisema mauzo yalikuwa madogo licha ya idadi kubwa ya wateja kujitokeza.

“Wateja walijitokeza lakini walinunua bidhaa za kawaida tu hivyo hakukuwa na ongezeko la mauzo. Hii ni ithibati kwamba Wakenya wanakabiliwa na hali ngumu,” akasema Bw Githua.

Wauzaji wa nguo ambao kwa kawaida huuza bidhaa nyingi wakati wa msimu wa sherehe za Krismasi, walisema kuwa mauzo yalikuwa duni.

“Yaani tunaweza kungojea kwa zaidi ya saa moja bila mteja kutokea. Biashara ya nguo na viatu imekuwa mbovu tangu Juni mwaka huu,” akasema Lucy Jerusha, ambaye huuza nguo za watoto katika mtaa wa Moi Avenue.

Wafanyabiashara wengi wa mavazi walikuwa wakitarajia mauzo ya juu kiasi kwamba waliagiza bidhaa nyingi kwa ajili ya maandalizi ya sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

“Huwa ninaagiza bidhaa zangu kutoka China na inasikitisha kwamba mauzo yamekuwa duni,” akasema Esther Valentine, ambaye huuza mavazi ya watoto katika jumba la maduka la Sasa Mall.

“Mapato ni duni mno kiasi kwamba hela ninazopata ninazitumia kulipa kodi ya nyumba ya Sh40, 000 kwa mwezi. Sijapata faida yoyote,” akaongezea.

Uchumi wa Kenya ulikua kwa asilimia 5.6 kati ya Januari na Juni, mwaka huu. Katika kipindi sawa mwaka jana uchumi ulikua kwa asilimia 6.4.

Kutokana na hali ngumu ya uchumi kampuni mbalimbali za kibinafsi zimesitisha shughuli ya kuajiri wafanyakazi wapya.

Kampuni nyingi zilizoorodheshwa katika Soko la Ubadilishanaji Hisa (NSE) tayari yametoa onyo kuhusu kudorora kwa faida.

You can share this post!

Polisi vidosho sasa marufuku kuvaa wigi

Msitumie mavazi yetu asili kiholela – Wazee wa Agikuyu

adminleo