• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
KRISMASI: Wafanyabiashara wageuka matapeli Uhuru Park

KRISMASI: Wafanyabiashara wageuka matapeli Uhuru Park

Na GEOFFREY ANENE

MSEMO ‘kila soko halikosi mwendawazimu’ ulipata maana Sikukuu ya Krismasi pale wanabiashara waligeuka kuwa matapeli katika bustani ya Uhuru Park kufyonza maelfu ya familia zilizofika humo kujiburudisha.

Idadi kubwa ya watu waliofika katika bustani hiyo inasemekana ilikuwa kutoka jamii za kutoka magharibi mwa Kenya walioamua kusalia jijini Nairobi baada ya magari ya abiria kuongeza nauli kutoka ile ya kawaida ya kati ya Sh800 na Sh1000 na kufikia hata Sh3,000.

Juhudi za wakazi walioamua kufurahia siku hiyo muhimu ya Wakristu duniani kwa kutumia hela kidogo katika bustani ya Uhuru Park zilitatizika pale wafanyabiashara wengi walipoamua kutumia ujanja kuongeza mapato yao.

“Nilikuwa napita mtu mmoja aliyekuwa anapaka watu hina. Niliposikia ni Sh80 kupakwa hina vidole vyote vya miguu na mikono, niliamua kujithibitishia kwa kuuliza bei tena ili niwe na uhakika. Mfanyabiashara huyo alisisitiza kuwa atanipaka hina vidole vyangu vyote kwa Sh80.

“Hata hivyo, mambo yalibadilika alipomaliza kunipaka na kuitisha Sh400. Niliposema nilikuwa na Sh80 alizosema, alinitisha kuwa atanidhuru. Alinieleza kuwa sikusikia bei vizuri akisema kuwa kupakwa kidole kimoja ilikuwa Sh20.

“Kwa bahati nzuri, kuna watu waliokuwa wamesikia bei aliyoniambia ya kwanza. Walipoanza kunitetea, alisema kuwa sasa amenipunguzia hadi Sh200 na akakatalia hapo na ikanilazimu nimpe Sh200,” alisimulia mama mmoja.

Mteja mwingine pia alipigwa na butwaa alipoambiwa alipe Sh200 baada ya kutobolewa masikio yake.

“Kabla ya kutobolewa masikio, niliuliza bei nikaambiwa kutoboa masikio yote ni Sh50. Sikuamini nilipoambiwa nilipe Sh200 baada ya kutobolewa,” alisema dada mmoja, ambaye hata hivyo, aliongeza “nilikataa kata kata kulipa zaidi ya Sh50 nilizokuwa nimeambiwa mwanzoni.”

Mfanyabiashara mmoja wa treni za kubeba watoto kwenye bustani ya Uhuru Park naye alipoteza wateja baada ya kupandisha bei ya kuziabiri kutoka Sh100 hadi Sh200.

“Bei yake ya kwanza ilikuwa Sh100 kuabiri treni hizo. Hata hivyo, alipoona wateja ni wengi aliamua kuifanya maradufu. Hivyo, wateja hawakuwa na subira naye na wakamtoroka,” alisema mteja mmoja.  

You can share this post!

Mama mkwe abeba chupi za jombi Krismasi

Ruto atupia Kalonzo ndoano

adminleo