Kimataifa

Waigizaji washambuliwa kuhusisha Yesu na ushoga

December 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

WAIGIZAJI wanne waliponea kifo chupuchupu baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa kutoa filamu ya kumdunisha Yesu mkesha wa Krismasi jijini Rio de Janeiro, Brazil.

Kwa mujibu wa shirika la habari la nchini humo, Agencia Brasil, watu wasiojulikana walishambulia jumba walilokuwemo waigizaji hao wa kundi la Porta dos Fundos.

Waigizaji hao wanadaiwa kutoa filamu iliyomhusisha Yesu na ushoga, jambo ambalo liliwakera Wakristo wa nchini Brazil.

Kulingana na polisi, washambuliaji hao walirusha vilipuzi kwenye jumba hilo lakini maafisa wa usalama walifanikiwa kuzima moto huo.

“Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika shambulio hilo. Lakini maafisa wa usalama wanafanya uchunguzi kubaini kwa lengo la kunasa waliohusika,” ikasema taarifa ya polisi.

“Hatudhani kwamba washambuliaji hao walikuwa magaidi. Lakini lolote lawezekana na tunaendelea na uchunguzi kubaini ikiwa shambulio hilo lilikuwa la kigaidi au la,” ikaongezea taarifa ya polisi.

Maafisa wa usalama wanachunguza kubaini ikiwa shambulio hilo linahusiana na filamu yenye jina: “The First Temptation of Christ,” ambayo ilipeperushwa katika mtandao wa Netflix siku chache kabla ya sherehe za Krismasi.

Filamu hiyo ambayo inamhusisha Yesu na ushoga imezua ghadhabu kali nchini Brazil ambapo kuna idadi kubwa zaidi duniani ya waumini wa Kanisa Katoliki.

Watu zaidi ya milioni 2.3 wametia saini katika mtandao wa Change.org kushinikiza filamu hiyo itolewe katika mtandao wa Netflix. Lengo la kampeni hiyo ni kufikisha saini milioni 3.

Saini nyingine zinakusanywa kupitia mitandao mingineyo.

Mwana wa kiume wa Rais Jair Bolsonaro – Eduardo – ni miongoni mwa watu walioshutumu vikali filamu hiyo ya dakika 46 huku akiitaja kuwa ‘takataka’.

Rais Eduardo alijitenga na filamu hiyo huku akisema kuwa haiwakilishi mtazamo na msimamo wa raia wa Brazil.

Kundi la Porta dos Fundos lina mashabiki milioni 16 katika mtandao wake na limejitokeza kushutumu serikali ya Brazil kwa ‘kuwanyima’ uhuru wasanii.

Mtandao wa Netflix ambao umetaja filamu hiyo kama ‘filamu spesheli ya Sherehe za Krismasi haijatoa taarifa yoyote licha ya kuwepo kwa shinikizo za kuutaka kuitupilia mbali.

Porta dos Fundos limeshikilia kuwa litaendelea kutoa filamu bila woga.

“Tumekuwa jasiri zaidi na tutaendelea kushirikiana na kuhakikisha kuwa tunamudu mawimbi ya chuki. Uhuru wa kujieleza ni sharti uzingatiwe na wote na upendo udumu,” wakasema waigizaji hao.