• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
MATUKIO 2019: BBI ilivyobadilisha mkondo wa siasa za Kenya mwaka huu

MATUKIO 2019: BBI ilivyobadilisha mkondo wa siasa za Kenya mwaka huu

Na CHARLES WASONGA

SIASA katika mwaka huu wa 2019 kwa kiasi kikubwa ziliathiriwa na shughuli za jopo la maridhiano (BBI) lililobuniwa baada ya mwafaka wa maelewano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga Machi 9, 2018.

Chini ya uongozi wa Seneta wa Garissa Yusuf Haji, jopo hilo la watu 14 limekuwa likizunguka kote nchini kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya kuhusu changamoto tisa zilizotambuliwa kama chimbuko la fujo ambazo zimekuwa zikishuhudiwa nchini kila baada ya uchaguzi mkuu.

Changamoto hizo pamoja na; ukabila, chaguzi za kuleta migawanyiko, ufisadi, usalama, ukosefu wa maadili ya kitaifa, ubaguzi katika teuzi za umma, ugatuzi kati ya nyingine.

Lengo la BBI lilikuwa ni kupendekeza mabadiliko ya kisera, kisheria na kikatiba zinazopasa kutekelezwa ili kushughulikia matatizo hayo ili yasichangie fujo na ghasia katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mwaka wa 2022.

Jopo kazi hilo liliwasilisha ripoti yake rasmi kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga mnamo Novemba 5. Hata hivyo likaongezwa muda baada ya maswali kadhaa kuibuliwa kutokana mapendekezo ya ripoti yake, haswa kuhusu suala nyeti la muundo wa uongozi.

Lakini kubuniwa BBI kuligawanya ulingo wa siasa kuwili; kati ya mrengo uliounga mkono jopo kazi hilo na uliolipinga.

Wanasiasa waliounga mkono jopo ni wale ambao walishabikia mwafaka (maarufu kama handisheki) kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga na ambao walishikilia kuwa hatua hiyo ilirejesha amani baada ya ghasia na uhasama zilizoshamiri nchini baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Hii ni pale Odinga ambaye alikuwa mgombeaji wa urais chini ya mwavuli wa muungano wa upinzani (Nasa) kupinga matokeo ya urais, akidai haki haikutendeka.

Wabunge, wanaoshabikia handisheki walibuni jina, ‘Kieleweke’ kwa ajili ya kujitambulisha kutokana na sababu kwamba wanatoka mirengo ya Jubilee na Nasa (hususan, chama cha ODM). Nyota wa mrengo huu ni Mbunge Maalum Maina Kamanda, mwenzake wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu, miongoni mwa wengine.

Wapinzani wa BBI ambao hutambuliwa kama ‘Team Tangatanga’ wanaamini kuwa ajenda kuu ya jopo hilo ilikuwa kuzima ndoto ya Naibu Rais William Ruto ya kuingia ikulu 2022.

Hii ndio maana wandani wa Dkt Ruto haswa kutoka eneo la Mlima Kenya na Rift Valley walisusia vikao vilivyoandaliwa na jopo hilo kukusanya maoni kutoka kwa umma katika maeno yao.

“Hatutahudhuria vikao vya BBI watakapofika hapa Murang’a kwa sababu tunaamini kuwa azma yao kuu ni kupendekeza kura ya maamuzi ili kumsaidia Raila kuingia uongozini 2022. Tuko nyuma ya Dkt Ruto kwa sababu tunaamini kuwa yeye ndiye anafaa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta kwa mujibu wa handisheki ya 2013,” akasema Mbunge wa Kandara Esther Wahome.

Kuchipuza kwa mrengo miwili ya kieleweke na Tangatanga kuhusiana na suala zima la BBI na handisheki kimsingi kulisababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya chama tawala, Jubilee, na mrengo wa upinzani.

Kwa mfano, katika eneo la Mlima Kenya hali ya vuta nikuvute kati ya wafuasi wa kundi la Tanganga na Kieleweke ilijitokeza mara kadhaa katika kaunti za Nyeri, Murang’a na Kirinyaga.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi wa Juni mkutano uliandaliwa na Mbunge Mwakilishi wa Nyeri Rahab Mukami na mwenzake wa Mathira Rigathi Gachagua, wa mrengo wa Tangatanga ulivurugwa na vijana waliodaiwa kuwa wafuasi wa Bw Wambugu, nyota wa Kieleweke.

Kiunjuri

Shughuli hiyo ya uzinduzi wa mradi wa maji katika eneo la Gatitu uliongozwa na Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri ambaye anasawiriwa kuegemea mrengo wa Naibu Rais.

Na katika eneo la Rift Valley, Dkt Ruto alikabiliwa na uasi mkubwa zaidi kutoka kwa wabunge waliounga mkono BBI na handisheki. Wao ni pamoja na; Joshua Kuttuny (Cherangany), William Kamket (Tiaty), Alfred Keter (Nandi Hills) na Silas Tiren (Moiben).

Wadadisi wanasema kuwa ni uhasama huu ambao umepelekea Rais Kenyatta kudinda kuitisha Mkutano wa Kundi la Wabunge wa Jubilee (PG), licha ya shinikizo kutoka kwa mrengo wa Tangatanga.

Duru zilisema kuwa kiongozi wa taifa alikataa kuitisha PG baada ya kubaini kuwa baadhi ya wafuasi wa Dkt Ruto walipanga kutumia jukwaa kama hilo kukosoa ushirikiano kati yake na Bw Odinga wanaohisi inahujumu nafasi ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.

Migawanyiko ndani ya Jubilee pia ilidhihirika ndani ya bunge, hali iliyompa Rais Kenyatta nafasi murua kwake kupitisha ajenda zake pasi na pingamizi kali.

Hii ni kwa sababu wabunge wa ODM na vyama tanzu katika muungano wa Nasa waliunga mkono miswada na sera zote kutoka Afisi ya Rais, baadhi yazo zikiwa zenye madhara kwa Wakenya na uchumi wa nchi.

Kwa mfano, katika moyo wa BBI na handisheki, bunge lilishindwa kubatilisha pendekezo la Rais katika mswada wa Fedha wa 2019 ulipenyeza kipengele cha kubatilisha sheria iliyodhibiti riba ambazo benki hutoza wateja wake.

Na mnamo Oktoba bunge lilishindwa kuweka kando pendekezo la Serikali ya kuongeza kiwango cha madeni ambayo serikali inaweza kukopa kutoka Sh6 trilioni hadi Sh9 trilioni.

You can share this post!

Jiji la Nairobi limesakamwa na majitaka, ripoti yafichua

Bidco Africa yawajali wagonjwa Thika

adminleo