• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
MATUKIO 2019: Uhuru wa mahakama ulitishiwa pakubwa

MATUKIO 2019: Uhuru wa mahakama ulitishiwa pakubwa

Na BENSON MATHEKA

KATIKA mwaka wa 2019, tulishuhudia mgogoro kati ya serikali kuu na idara ya mahakama uliofikia kilele Jaji Mkuu David Maraga alipodai baadhi ya mawaziri walikuwa na njama za kumtimua mamlakani.

Kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kusimamia mahakama na pengine mara ya kwanza katika historia ya Kenya kwa afisa wa cheo chake, Jaji Mkuu Maraga, alishambulia serikali kwa kutaka kunyima mahakama uhuru wake.

Hii ilikuwa ni baada ya serikali kupunguza bajeti ya idara ya mahakama na majaji kulaumiwa kwa kulemaza vita dhidi ya ufisadi, madai ambayo Bw Maraga alikanusha vikali.

Kila alipopata nafasi kuzungumzia vita dhidi ya ufisadi, Rais Uhuru Kenyatta alilaumu mahakama kwa kuwa kizingiti katika juhudi za serikali yake kukabiliana na uovu huo.

Licha ya Bw Maraga kufafanua changamoto ambazo idara yake hupitia kusikiliza kesi na kuamua kesi, Rais Kenyatta aliongoza wakuu wa idara zinazohusika na haki kushambulia mahakama.

Mgogoro huo ulifikia kilele bajeti ya mahakama ilipopunguzwa mapema Septemba kwa Sh3 bilioni

Ilibidi Bw Maraga kuitisha kikao cha wanahabari na kutangaza kuwa huduma katika mahakama zingekwama baada ya serikali kupunguza bajeti yake.

Wakenya walielekezea Rais Uhuru Kenyatta kidole cha lawama wakisema alikuwa akitimiza vitisho vyake vya kuadhibu majaji kwa kubatilisha ushindi wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Mbali na kunyimwa pesa, Jaji Mkuu Maraga alilalama kuwa alikuwa akidharauliwa na maafisa serikalini, ambao alidai walipanga njama Rais kuteka usimamizi wa Idara ya Mahakama.

Bila kutaja majina, Jaji Maraga alisema kuna mawaziri na makatibu wa wizara ambao waliapa kumng’oa mamlakani.

“Kumbe hii nchi ina wenyewe! Acheni niwaambie, niko hapa kutekeleza wajibu niliopewa na wananchi. Sikuajiriwa na waziri wala katibu wa wizara,” alisema na kuapa kutojiuzulu.

Alisisitiza hatajiuzulu ikiwa hilo ndilo lengo la wanaomhujumu bali ataendelea kutetea haki na uhuru wa mahakama.

Alidai mawaziri kadhaa wamemdharau kiasi cha kwamba hawawasiliani naye moja kwa moja bali hutumia makarani kumwandikia barua, ambazo alisema yeye huzirarua kwani hawezi kuvumilia kudharauliwa kiasi hicho.

Anaposafiri kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Jaji Mkuu anasema huwa maafisa hawataki atumie chumba cha wageni waheshimiwa wakidai kimetengewa Naibu Rais William Ruto pekee.

“Nimeamua nisipoheshimiwa kama ipasavyo, sitakuwa nikihudhuriabaadhi ya hafla za kitaifa. Ninaposafiri nje ya nchi huwa napewa taadhima tele. Hapa naambiwa hata chumba cha wageni waheshimiwa siruhusiwi kuingia,” akasema.

Akosa kuhudhuria sherehe za Jamhuri

Na kama hatua ya kuthibitisha kwamba hakuwa akifanya mzaha, Bw Maraga hakuhudhuria sherehe za 2019 za Jamhuri katika uwanja wa michezo wa Nyayo jijini Nairobi.

Wakenya wa matabaka mbali mbali walimuunga mkono wakilaumu serikali kwa kunyima mahakama pesa.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli alimtaka Rais Kenyatta kuingilia kati akisema Serikali haifai kuingiza siasa katika utoaji haki.

Nayo Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC) ilikashifu wizara ya fedha kwa kupunguza mgao wa fedha kwa Idara ya Mahakama ikisema hatua hiyo ilifaa kuidhinishwa na bunge la kitaifa.

You can share this post!

Wataenda wapi wahasiriwa wa mafuriko Januari?

MATUKIO 2019: Watu mashuhuri walioacha pengo baada ya...

adminleo