Habari Mseto

Maporomoko ya ardhi na mafuriko yasababisha uharibifu Machakos

December 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY KIMATU

WAKAZI katika vijiji vya Mutituni, Sinai na Ngelani katika Kaunti ya Machakos wanakadiria hasara baada ya mafuriko ya hivi karibuni yanayowakosesha usingizi.

Wanatoa wito kwa viongozi kushughulikia suala la maporomoko ya ardhi katika kijiji cha Sinai kuteremka hadi karibu na barabara ya Kisekini -Ngelani.

Kuteleza kwa ardhi kuliacha shimo kubwa ambalo ni la zaidi ya futi 50 kwa kina na la urefu wa takriban nusu kilomita.

Wakazi wanaofia maisha yao kwani wanakabiliwa na hatari kubwa kwani mmomonyoko wa udongo katika kilima cha Sinaim kwenye eneo la Ngelani unaendelea kila siku mvua inyeshapo.

Barabara ya Ngelani-Sinai-Yakamete pia inatishiwa na maporomoko hayo kwani imebakia mita tano ifikiwe.

Wale wanaoishi karibu na eneo la kisa wameamua kuhamia kwa majirani zao wakitafuta kimbilio.

Wakati huo huo katika eneo tambarare la Inyooni lililopo kando ya barabara ya kuunganisha Mutituni-Musilili-Kiteini imeharibiwa na mvua.

Ni barabara iliyoharibika hasa kwenye daraja la Inyooni na kufanya iwe vigumu kwa wanatumiaji.

Mwakilishi wa Wadi ya Mutituni, Bw Johana Munyao ambaye alilaumu wavunaji wa mchanga kwa kuchangia daraja iliyoharibiwa wakati wenyeji wanawalaumu viongozi wa kisiasa kwa shida hiyo.

Sehemu ya barabara imeathiriwa na mmomonyoko wa ardhi huku nusu yake ikibakia kuwa nyembamba kwa watembeao kwa miguu na waendeshaji bodaboda.

Barabara iliyoathiriwa na mmomonyoko wa ardhi katika kijiji kimojawapo Kaunti ya Machakos. Picha/ Sammy Kimatu

Walioathirika zaidi ni wakulima wa mboga, wakulima wa parachici na wakuzaji kahawa. Barabara inaunganisha wakulima na Kiwanda cha kahawa cha Musilili na Kituo cha biashara cha Mutituni.

Mafuriko hayo yalisababishwa na maji ya mafuriko kutoka Mua Hills, Ngelani, Yumbani na vilima vya Kisekini.