• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Mshtuko kwa wazazi baada ya karo kupanda

Mshtuko kwa wazazi baada ya karo kupanda

Na FAITH NYAMAI

WAZAZI wanakabiliwa na mshtuko kuhusu nyongeza ya karo ya shule huku shule zikifunguliwa kwa muhula wa kwanza.

Licha ya serikali kudhibiti karo, walimu wakuu wa shule wanatafuta mbinu nyinginezo za kuongeza karo kupitia ada nyingi wanazotoza wazazi.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wazazi Nicholas Maiyo alieleza ‘Taifa Jumapili’ kwamba wazazi wengi wamestaajabu huku wakilazimika kuwalipia watoto wao ada hizo za ziada.

Bw Maiyo alisema nyongeza hiyo katika karo ya shule ni kinyume na maelekezo yaliyowekwa na Wizara.

Bw Maiyo alisema amepokea malalamishi kutoka kwa wazazi wengi huku mzazi mmoja akiripoti kwamba mwalimu mkuu wa shule ya msingi mojawapo alikuwa ameitisha Sh20,000 ili kumsajilisha mwanafunzi katika shule yake.

“Baadhi ya walimu wakuu wanatumia vibaya sare na miundomsiungi ya shule kujinufaisha kwa kuwataka wazazi kulipa karo ya ziada,” alisema.

Wengine wanaitisha pesa za kuwapa wanafunzi uhamisho huku wengine wakiwataka wanafunzi wanaofuzu kutoka shule za chekechea hadi gredi ya kwanza kulipa ada za dharura za kiasi cha hadi Sh2000 licha ya kulipa kiasi sawa na hicho mwaka uliopita.

Wazazi waliozungumza na ‘Taifa Jumapili’ walifichua kwamba shule zinawaagiza wazazi kulipa ada hizo za ziada kupitia akaunti tofauti na ile inayotumika kwa karo ya shule.

Wizara ya Elimu huwaruhusu walimu wakuu was shule kufungua akaunti za benki za kulipia karo za shule na ufadhili wa serikali.

Akaunti hizo hukaguliwa na maafisa wa elimu nyanjani kuhakikisha uadilifu.

Hata hivyo, kwa akaunti hizo mbadala, wazazi walifichua kuwa walimu wakuu huziweka kisiri.

Katika baadhi ya shule za sekondari, wazazi waliripoti kuwa walimu wakuu wamewataka wazazi kulipa kiasi cha Sh5000 hadi Sh7000 kugharamia sare za shule.

Bw Maiyo alitaja hatua hiyo kama njama za kuwapunja wazazi kupitia karo zaidi.

Alisema wazazi hawatalipa karo yoyote ya ziada kando na ile iliyotolewa na wizara ya elimu.

“Walimu wakuu wa shule hawapaswi kuwatumia vibaya wazazi ili kujinufaisha kwa kuitisha karo zaidi,” alisema.

Bw Maiyo alisema muungano huo unakusanya habari kutoka kwa wazazi na kwamba shule yoyote itakayokiuka utaratibu kuhusu karo itaripotiwa kwa wizara.

Muungano wa walimu pia umepinga pendekezo la Mwenyekiti wa Muungano wa Walimu Wakuu katika Shule za Sekondari (Kessha) Kahi Indimulli kwa Wizara ya Elimu akiomba karo ya shule iongezwe.

Walimu wakuu waliomba kwamba shule katika kaunti zilipe Sh17, 000 zaidi huku shule ambazo si za bweni zikilipa Sh6000 zaidi.

Wazazi wenye watoto katika shule za kaunti watalipa Sh7, 537 zaidi.

Wazazi kadhaa jana walisema walimu wakuu wanaitisha ada za masomo ya ziada, miundomsingi, maendeleo na dharura kwa wanafunzi wanaoendelea.

Mzazi mmoja jana alisema sare inayouzwa shuleni ni ya kiwago duni hivyo kuwalazimu wazazi kununua sare mpya kila mara.

You can share this post!

Kenya kusutwa na AU kuhusu maskwota wa Mau

MWANASIASA NGANGARI: Mzee Moi: Mlezi wa vigogo wa kisiasa...

adminleo