• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 3:23 PM
Misongamano yashuhudiwa katika vituo vya uchukuzi wa umma nauli ikipanda

Misongamano yashuhudiwa katika vituo vya uchukuzi wa umma nauli ikipanda

Na SAMMY WAWERU

WAHUDUMU wa matatu katika vituo mbalimbali Jumatatu waliongeza nauli karibu maradufu kufuatia idadi kubwa ya watu iliyoshuhudiwa.

Ni hali inayotarajiwa kuendelea wiki hii, hasa shule zinapofunguliwa muhula wa kwanza 2020. Pia, kuna watu wanaorejea mijini kutoka likizo ya mwezi Desemba 2019.

Kinyume na inavyokuwa msimu wa Krismasi, nauli kuongezeka kuelekea mashambani, pande zote; kuelekea mashambani na mijini wiki hii, inatarajiwa kuwa ghali kwa sababu ya wanafunzi.

Mjini Thika kuelekea jijini Nairobi, jana wasafiri hawakuwa na budi ila kulipa mara dufu.

“Kituo hiki kuelekea Nairobi nauli huwa kati ya Sh50 – 70, leo ni Sh100,” akalalamika Salome Wainaina, anayefanya kazi jijini Nairobi japo anaishi mjini Thika.

Kulingana na Bi Salome wahudumu wa matatu wanatumia mwanya wa watu kurejea mijini na wanafunzi shuleni, kunyanyasa wasafiri.

“Ninashangaa kwa nini watuongezee nauli ilhali sisi ni wateja wa kila siku,” akaambia ‘Taifa Leo’.

Jijini Nairobi, kuelekea maeneo kama vile Embu, Meru, Kirinyaga na Nyeri, taswira ni ile ile. Kwa mfano, nauli kati ya Nairobi na Nyeri huwa kadri ya Sh300, lakini kufikia jana jioni ilikuwa Sh500.

“Magari yakirudi Nairobi ni vigumu kupata wasafiri, hivyo basi hatuna budi ila kusawazisha kwa kuongeza nauli,” akasema mhudumu wa matatu jijini Nairobi.

Hali si tofauti mjini Eldoret, ambapo nauli kuelekea Nairobi imepanda kutoka Sh700 hadi Sh1, 200 na kusababisha msongamano wa wasafiri. Lawi Kimeli, mkazi, aliambia ‘Taifa Leo’ kwa kwamba uhaba wa magari pia unashuhudiwa humo vituoni.

Bw Simon Muchangi, ambaye bintiye anasomea mjini Nyeri amelalamikia ongezeko la nauli ikizingatiwa kuwa gharama ya maisha inaendelea kukwea mlima kila uchao.

“Mvulana wangu wiki ijayo anatarajia kujiunga na kidato cha kwanza, nina msichana aliye chuo kikuu aliyeenda Jumatatu. Ni nauli nitalipia wanavyotaka au ni karo? Uchumi umekuwa ghali,” amesema mzazi huyo, akiirai serikali kudhibiti sekta ya matatu.

Muhula wa kwanza kila mwaka huwa na gharama yake, hususan kwa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza. Ni muhula ambao karo huwa ghali, bila kusahau mahitaji ya watoto shuleni.

You can share this post!

Ripoti ya UNDP yaonyesha idadi ya vifo vinavyosababishwa na...

WASONGA: Utekelezaji duni wa sera umetatiza sekta ya madini

adminleo